Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ayuatullah Khamenei:

Jinai ya baharini ya utawala wa Kizayuni wa Israel ni dalili ya kuchanganyikiwa utawala huo ghasibu

Kufuatia jinai na shambulizi la kinyama lililofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Msafara wa Uhuru uliokuwa umebeba misaada ya kibinadamu kwa ajili ya wananchi wa Ukanda wa Gaza, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei leo ametoa ujumbe akiitaja jinai hiyo kuwa ni shambulizi dhidi ya ubinadamu kote duniani. Ayatullah Khamenei amesema: "Leo hii Palestina si suala la Waarabu au hata Waislamu pekee, bali ni kadhia inayohusu haki za binadamu za dunia ya sasa, na waungaji mkono wa utawala wa Kizayuni wa Israel hususan Marekani, Uingereza na Ufaransa wanapaswa kuwajibika vilivyo katika suala hilo."

Matini kamili ya ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni hii ifuatayo:

Bismillahir Rahmanir Rahim.

Jinai na na shambulizi la kikatili la utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya msafara wa meli zilizokuwa na misaada ya kibinadamu, ni sehemu ya mnyororo wa jinai kubwa zilizorundikana kwenye faili la jinai za utawala huo mshari na khabithi katika muongo huu wa saba wa maisha yake yaliyojaa nakama. Huu ni mfano wa wazi wa vitendo vya jeuri na visivyo na chembe ya huruma ambavyo wanatendewa Waislamu wa eneo hili hususan kwenye ardhi madhulumu za Palestina kwa makumi ya miaka sasa. Mara hii msafara huo haukuwa wa Kiislamu wala wa Kiarabu bali ulikuwa ni wa watu wenye utu na ubinaadamu kutoka kona mbalimbali za dunia. Bila ya shaka shambulizi hilo la kijinai limewatimizia hoja watu wote kwamba Uzayuni ni sura mpya ya ukatili mkubwa zaidi kuliko ufashisti ambayo hivi sasa inaoneshwa na Wazayuni kwa uungaji mkono na msaada wa madola yanayodai kupigania uhuru na haki za binaadamu yakiongozwa na serikali ya Marekani.

Marekani na Uingereza, Ufaransa na madola mengine ya Ulaya yanaunga mkono jinai hizo ambazo ni dhati ya Wazayuni kwa kutumia hila za kisiasa, vyombo vya habari, jeshi na uchumi. Siku zote madola hayo yako nyuma ya maafa yanayofanywa na Wazayuni, hivyo yanapaswa kutoa majibu ya kina na yabebe jukumu la jinai za Wazayuni hao. Watu wenye hisia za utu katika kila kona ya dunia wanapaswa kutafakari na kuona jinsi ubinaadamu leo hii unavyotishiwa na hali ya hatari kabisa katika eneo nyeti ya Mashariki ya Kati. Waone ni kiasi gani utawala wa kiwendawazi, wa kikatili na wa umwagaji wa damu unavyoikalia kwa mabavu nchi ya Palestina na kuwafanyia ukatili mkubwa wananchi madhulumu wa ardhi hizo. Kwa miaka mitatu sasa watu milioni moja na nusu, wanawake na watoto wadogo wa Gaza wamezingirwa na Wazayuni na kufungiwa njia zote wa kuingiza vyakula, madawa na kuendeshea maisha yao ya kila siku. (Watu wenye fikra huru wakae na kufikiria) ni nini maana ya jambo hilo. Mtu anaweza kuyaeleleza vipi mauaji, vifungo na mateso ya kila leo wanayofanyiwa vijana wa Gaza na wa Ukingo wa Magharibi?

Hivi sasa tena kadhia ya Palestina si kadhia ya Kiarabu tu wala si suala la Kiislamu tu, bali imekuwa ni kadhia muhimu mno katika suala zima la haki za binaadamu kwenye ulimwengu wetu huu.

Kazi ya kupigiwa mfano na ya kupongezwa ya kupelekwa msafara wa meli huko Gaza inabidi iendelee kwa mara nyingi na kwa makumi ya sura na mbinu tofauti. Utawala katili wa Kizayuni na waungaji mkono wake hasa Marekani na Uingereza bila ya shaka sasa wanaiona na kuihisi nguvu isiyoshindika ya azma, nia ya kweli na mwamko wa hisia za kibinaadamu kote ulimwenguni.

Tawala za nchi za Kiarabu nazo ziko katika mtihani mgumu hivi sasa. Wananchi walioamka wa nchi za Kiarabu wanataka kuona tawala zao zinachukua hatua madhubuti na zisizotetereka dhidi ya Wazayuni. Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC) na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) hazipaswi kutulia ila baada ya kuhakikisha kuwa mzingiro wa Gaza umeondolewa kikamilifu, kumekomeshwa kitimilifu uporaji wa nyumba na ardhi za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi pamoja na kuhakikishwa kuwa wamepandishwa kizimbani watenda jinai kama vile Netanyahu na Ehud Barak.

Taifa lenye kupigana jihadi la Palestina na wananchi na serikali ya kidemokrasia ya Gaza nayo inapaswa kujua kuwa, adui yao khabithi hivi sasa amedhii na kudhoofika mno. Shambulizi la baharini lililofanywa na Wazayuni siku ya Jumatatu si tu si ishara ya kuwa na nguvu, bali hata ni ushahidi wa kuchanganyikiwa na kuemewa utawala huo ghasibu. Suna ya Mwenyezi Mungu imethibiti tena hapa kwamba madhalimu wako mwishoni mwa njia yao iliyojaa nakama na wanajipeleka kwa mikono yao kwenye hatima yao ya maangamizi na kutoweka kabisa. Shambulizi dhidi ya Lebanon na baadaye katika Ukanda wa Gaza yaliyofanywa kwenye miaka ya huko nyuma ni miongoni mwa hatua hizo za kipunguwani ambazo zimewaburuta magaidi wa Kizayuni karibu kabisa na shimo la kuangamia. Shambulio dhidi ya msafara wa kimataifa wa misaada katika maji (ya kimataifa ya bahari) ya Mediterranean nalo ni hatua nyingine ya kiwendawazimu mithili ya hatua za huko nyuma.

Makaka na madada wa Palestina! Mtegemeeni Mwenyezi Mungu Mwingi wa hekima, Mwenye nguvu. Ziaminini nguvu zenu na ziongezeni mbinde, nguvu hizo. Kuweni na yakini kuwa hatima ya yote, ushindi ni wenu nyinyi. Jueni kuwa:


وَلَيَنصُرَنَّ اللَّـهُ مَنْ يَنصُرُهُ إِنَّ اللَّـهَ لَقَوِيٌّ عَزِيزٌ.


(Na bila ya shaka Mwenyezi Mungu humsaidia yule anayemsaidia Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mtukufu)

Sayyid Ali Khamenei

11 Khordad 1389 (01 Juni 2010).


700 /