Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu kwa mnasaba wa siku ya saba tangu kuuawa shahidi makumi ya wananchi wa Zahedan

Taasisi zote husika zinapaswa kuwapa wafitini jaza yao kwa uhalifu waliotenda

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei leo ametoa ujumbe kwa mnasaba wa kutimia siku ya saba tangu kuuawa shahidi makumi ya wananchi waumini wa mji wa Zahedan huko kusini mashariki mwa Iran katika milipuko ya kigaidi iliyolenga msikiti mkuu wa mji huo akivitaja vyombo vya ujasusi vya Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel na Uingereza kuwa ndio wahusika wakuu wa jinai hiyo. Ayatullah Khamenei amesema kuwa moja ya malengo makuu ya maadui katika kutekeleza shambulio hilo la kigaidi ni kuzusha hitilafu na fitina za kimadhehebu lakini Jamhuri ya Kiislamu haitaruhusu mikono ya ubeberu wa kimataifa kufikia lengo lake. Vilevile amevitaka vyombo vyote husika vya Serikali, Bunge na Mahakama kupambana vilivyo na maadui wa umoja na usalama wa taifa na kuwafikisha wahalifu mbele ya sheria.

Ujumbe kamili wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni huu ufuatao:

Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehma Mwenye kurehemu

Siku ya saba tangu kuuawa shahidi kidhulma baadhi ya wananchi wenzetu waumini na wenye ikhlasi huko Zahedan ambao wameuawa na wahalifu na magaidi wasokuwa na huruma, imewadia. Katika tukio hilo la umwagaji damu, mikono ya wahalifu waliopotoka na mawahabi wenye chuki za kimadhebehu ambao wanasaidiwa na kuchochowe na mashirika ya kijasusi ya kigeni imezitia simanzi na msiba nyoyo na familia ambazo taa ya mahaba na upendo kwa Watu wa Nyumba ya Mtume imekuwa ikiwaka ndani yake na nuru ya maarifa na kumpwekesha Mwenyezi Mungu imezimulikia.

Wahalifu hao wenye chuki za kimadhehebu, vipofu, majahili na wauaji wamezikabidhi nyoyo zao zilizopotea na nafsi zao zilizojaa giza kwa madola maovu ambayo yamekuwa yakionesha uadui wao dhidi ya Uislamu mara kwa mara, na kila mara na mahala zimedhihirisha ufidhuli na chuki yao kwa Waislamu na kuwahujumu.

Uadui wa madola hayo pia dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unatokana na kupeperushwa bendera ya Uislamu katika nchi hii na wito wake wa siku zote wa kulingania umoja, nguvu na heshima ya Kiislamu.

Moja ya melengo ya maadui katika tukio hilo la umwagaji damu na matukio mengine kama hayo ni kuzusha hitilafu kati ya Waislamu. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo kwa miongo kadhaa imekuwa mtetezi mkubwa zaidi na wa kuaminika wa Waislamu wanaodhulumiwa huko Gaza, Palestina yote, Afghanistan, Kashmir na maeneo mengine ya Kiislamu, sasa inalengwa kwa njama hizo chafu za mashirika ya kijasusi ya Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel na Uingereza ili kwa fikra zao finyu itumbukie katika fitina za kimadhehebu na ugomvi baina ya Shia na Suni. Maadui hao wameghafilika kwamba Wasuni katika Iran ya Kiislamu kama walivyo ndugu zao wa Kishia, wamethibitisha mara kwa mara uaminifu wao kwa utawala mtukufu wa Kiislamu na kusimama kidete kishujaa na kwa imani mbele ya ubeberu na vibaraka wake kwa ajili ya kuilinda Jamhuri ya Kiislamu na nchi yao azizi ya Iran.

Kimsingi, kutokea na kukua kwa ugaidi kipofu katika eneo hili ni matokeo ya siasa zilizojaa uhabithi za Marekani, Uingereza na vibaraka wao wa kiserikali na usiokuwa wa kiserikali; kwa msingi huo ni wajibu kwa Waislamu wote kupambana na mwanaharamu huyo najisi ambae ni kilelelezo kikubwa cha kueneza ufisadi katika nchi na kumpiga vita Mwenyezi Mungu.

Makundi yote ya Ahlusunna nchini Iran na katika nchi jirani ambayo heshima na hadhi yao ya Kiislamu inashambuliwa kwa siasa hizo habithi hususan wanazuoni wa kidini, wasomi na wahadhiri wa vyuo vikuu, wana wajibu mzito zaidi.

Wasomi wa Kishia na Kisuni katika nchi zote za Kiislamu na Kiarabu wanapaswa kuweka wazi na kubainisha malengo maovu ya maadui katika kuanzisha na kuimarisha ugaidi wa kimakundi na kuwatahadharisha watu kuhusu hatari kubwa ya fitina za kimadhehebu ambazo ndio matumaini makubwa ya maadui wa Uislamu.

Kwa idhini yake Mola Muweza, Jamhuri ya Kiislamu haitairuhusu mikono ya ubeberu wa kimataifa kuzusha hitilafu kati ya Waislamu kwa kutumia jina la mawahabi na wengineo kama wao. Vyombo vyote husika vya Serikali, Bunge na Mahakama vinawajibika kupambana vilivyo na maadui wa umoja na usalama wa taifa na kuwafikisha wahalifu mbele ya sheria. Vilevile wananchi wenye imani wanapaswa kulinda utulivu na kuwa na umaizi na kuwasaidia maafisa husika wa nchi kutekeleza vyema majukumu yao kwa kujiepusha na harakati yoyote isiyokuwa ya kimantiki.  

Kwa mara nyingine tena ninatuma salamu zangu kwa roho za mashahidi waliouawa katika shambulizi hilo la umwagaji damu lililofanyika sambamba na maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Bwana wa Mashahi Imam Hussein (as) na ninatuma salamu za rambirambi kwa familia zao nikizitaka kuwa na subira na utulivu na kuziombea ujira na malipo mema kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Vilevile ninamuombea Mwenyezi Mungu Mtukufu awape shufaa ya haraka watu waliojeruhiwa katika tukio hilo.

Salamu, rehema na baraka za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya waja wake wema.

Sayyid Ali Khamanei

30/Tir 1389 (21 Julai 2010)

700 /