Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu asema katika ujumbe muhimu kwa umma wa Kiislamu:

Serikali ya Marekani inapaswa kuwaadhibu ipasavyo wahusika wakuu wa jinai hii kubwa

Kufuatia kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur’ani Tukufu nchini Marekani, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ametoa ujumbe muhimu kwa taifa la Iran na umma mkubwa wa Kiislamu akitaja makundi ya Kizayuni ndani ya serikali ya Marekani kuwa ndiyo yaliyopanga njama hiyo ya kuchukiza. Ayatullah Khamenei amebainisha malengo ya siri ya chuki za Wazayuni dhidi ya Uislamu na Qur’ani akisisitiza kuwa: “Ili kuthibitisha madai yake kwamba haikuhusika katika njama hiyo, serikali ya Marekani inawajibika kuwaadhibu ipasavyo wahusika wakuu na watekelezaji wake.” Matini kamili ya ujumbe wa Walii amri wa Waislamu duniani ni hii ifuatayo:

Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehma, Mwenye kurehemu

Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: “Hakika Sisi ndio tulioteremsha Qur’ani hii, na Sisi ndio tutakaoilinda.”

Taifa azizi la Iran, umma mkubwa wa Kiislamu!

Dharau ya kiendawazimu na yenye kuchukiza iliyofanywa nchini Marekani dhidi ya Qur’ani chini ya ulinzi wa polisi ya nchi hiyo ni tukio chungu na kubwa ambalo haliwezi kuhesabiwa kuwa ni harakati ya kijinga ya watu kadhaa vibaraka na wasiokuwa na thamani yoyote. Hii ni hatua iliyofanyika kwa mahesabu maalumu na vituo ambavyo tangu miaka kadhaa iliyopita vimekuwa vikitekeleza siasa za kuwatia watu hofu kuhusu Uislamu na kuihujumu dini hiyo. Vituo hivyo vimekuwa vikiushambulia Uislamu na Qur’ani kwa kutumia mamia ya mbinu na maelfu ya nyenzo za kipropaganda. Tukio hili ni sehemu ya mnyororo wa fedheha ulioanza kwa hiana ya murtadi Salman Rushdi na kudumishwa kwa harakati za mchora vibonzo habithi wa Demnark  na makumi ya filamu zilizotengenezwa dhidi ya Uislamu huko Hollywood na sasa umefikia katika mchezo huu uliojaa chuki na uhasama.

Je, ni nani na kitu gani kilicho nyuma ya pazia la harakati hii iliyojaa shari na uovu?

Utafiti kuhusu mwenendo huo wa uovu na shari ambao katika miaka ya sasa umeandamana na vitendo vya jinai na uhalifu huko Afghanistan, Iraq, Palestina, Lebanon na Pakistan, haubakishi shaka yoyote kwamba wapangaji na vituo vya kuongoza harakati hizo vinamilikiwa na viongozi wa mfumo wa kibeberu na vituo vya kifikra vya Kizayuni ambavyo vina ushawishi mkubwa zaidi katika serikali ya Marekani na taasisi zake za kiusalama na kijeshi na pia katika serikali ya Uingereza na baadhi ya nchi za Ulaya. Hao ndio walewale ambao siku baada ya nyingine uchunguzi huru wa kutafuta ukweli unawaelekezea vidole vya tuhuma za kuhusika na mashambulizi ya Septemba 11. Mashambulizi hayo yalimpa rais mtenda jinai wa wakati huo wa Marekani kisingizio cha kuzishambulia kijeshi nchi za Afghanistan na Iraq na kutangaza Vita vya Msalaba; na kwa mujibu wa ripoti kadhaa, mtu huyo huyo jana alitangaza kwamba vita hivyo vya msalaba sasa vimeshika kasi baada ya kanisa kuingia katika medani.

Lengo la hatua ya sasa ya kuchukiza kwa upande mmoja ni kupanua duara la vita dhidi ya Uislamu na Waislamu katika jamii ya Kikristo na kulifikisha katika kiwango cha wananchi wote na kuvipa sura ya kidini kwa kuingia kanisa na makasisi katika vita hivyo na kuungwa mkono kwa chuki na hisia za kidini. Katika upande mwingine hatua hiyo inalenga kuyasahaulisha mataifa ya Kiislamu yaliyokasirishwa na kuumizwa mno na kiburi hicho kikubwa na kuyaghafilisha na masuala ya dunia ya Kiislamu na Mashariki ya Kati.

Hatua hiyo iliyojaa chuki na uhasama si mwanzo wa harakati bali ni awamu nyingine ya mwenendo wa muda mrefu wa kuuhujumu Uislamu unaoongozwa na Uzayuni na utawala wa Marekani. Kwa sasa viongozi wote wa ubeberu na vinara wa ukafiri wamesimama katika safu moja ya kuupiga vita Uislamu. Uislamu ni dini ya uhuru na masuala ya kiroho ya mwandamu na Qur’ani ni kitabu cha rehma, hikima na uadilifu. Ni wajibu wa wapigania uhuru kote duniani na dini zote za mbinguni kusimama pamoja na Waislamu katika kukabiliana na siasa chafu za kuuhujumu Uislamu kwa kutumia mbinu hizo za kuchukiza. Viongozi wa utawala wa Marekani hawawezi kujivua tuhuma za kuhusika na tukio hilo ovu kwa kutoa matamshi ya hadaa na yasiokuwa na maana. Ni miaka mingi sasa ambapo matukufu, haki zote na heshima ya mamilioni ya Waislamu wanaokandamizwa huko Afghanistan, Iraq, Lebanon na Palestina zinakanyagwa. Je, malaki ya watu waliouawa, makumi ya maelfu ya wanawake na wanaume waliotekwa na kuteswa, maelfu ya watoto wadogo na wanawake waliotekwa nyara na mamilioni ya walemavu na watu walioharibiwa makazi yao ni wahanga wa kitu gani?

Kwa kutilia maanani dhulma hizo zote, ni kwa nini vyombo vya habari vya kimataifa vya nchi za Magharibi vinawadhihirisha Waislamu kuwa ni kielelezo cha ukatili na utumiaji mabavu na kwamba Qur’ani na Uislamu ni hatari kubwa kwa wanadamu? Ni nani anayeamini kwamba njama hiyo kubwa inaweza kufanyika bila ya msaada na uingiliaji wa duru za Kizayuni ndani ya serikali ya Marekani?

Ndugu Waislamu nchini Iran na duniani kote!

Ninaona wajibu kuwakumbusha masuala kadhaa yafuatayo:

1- Tukio hili na mengine ya kabla yake yanaonesha wazi kwamba Uislamu azizi na Qur’ani Tukufu ndivyo vinavyolengwa kwa mashambulizi ya mfumo wa ubeberu wa kimataifa. Vilevile uadui wa waziwazi wa mabeberu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unatokana na misimamo ya wazi ya Iran ya kukabiliana na mabeberu hao, na hila zao za kujidhihirisha kwamba hawana uhasama na Uislamu na Waislamu wengine ni urongo mkubwa na hila ya kishetani. Mabeberu hao ni maadui wa Uislamu na kila mtu anayeshikamana barabara na dini hiyo na kila nembo ya Kiislamu.

2- Mlolongo huu wa chuki na uhasama dhidi ya Uislamu na Waislamu unatokana na ukweli kwamba tangu miongo kadhaa iliyopita hadi sasa nuru ya Uislamu inang’ara zaidi na ushawishi wake katika nyoyo za watu katika dunia ya Kiislamu na hata katika nchi za Magharibi umeongezeka zaidi na zaidi. Uhasama huo unatokana na kwamba umma wa Kiislamu umeamka zaidi na mataifa ya Kiislamu yameazimia kukata minyororo ya ukoloni wa kipindi cha karne mbili ya uvamizi wa mabeberu. Tukio la kuvunjiwa heshima Qur’ani na Mtume Mtukufu (saw) licha ya kuwa chungu, lakini linabeba bishara kubwa. Jua lenye mwanga na nuru kubwa la Qur’ani litazidi kung’aa na kumulika zaidi siku baada ya siku.

3- Sisi sote tunapaswa kuelewa kwamba tukio la kuvunjiwa heshima Qur’ani halina uhusiano na kanisa wala Wakristo na harakati za kianasesere za makasisi kadhaa wapumbavu na vibaraka hazipaswi kuhusishwa na Wakristo na viongozi wao wa kidini. Sisi Waislamu kamwe hatutafanya matendo kama hayo dhidi ya matukufu ya dini nyingine. Maadui na wapangaji wa mchezo huo wa kuigiza na wa kiendawazimu wanataka kuzusha mivutano kati ya Waislamu na Wakristo katika jamii, lakini darsa na somo la Qur’ani kwetu sisi ni kinyume na jambo hilo.

4- Upande unaokabiliana na Waislamu wote hii leo ni serikali ya Marekani na wanasiasa wa nchi hiyo. Iwapo wanasema kweli katika madai yao ya kutohusika katika tukio la kuvunjiwa heshima Qur’ani basi wanawajibika kuwaadhibu ipasavyo wahusika halisi wa jinai hiyo kubwa na watekelezaji wake ambao wameziumiza mno nyoyo za Waislamu bilioni moja na nusu.

Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu ya waja wake wema

Sayyid Ali Khamenei

22 Shahrivar 1389 (13/09/10)             

700 /