Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ayatullah Khamenei asema katika ujumbe wake kwenye kikao cha taifa cha swala:

Mahudhurio ya vijana yanapaswa kutia nishati na kuhuisha misikiti

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran Ayatullah Ali Khamenei ametuma ujumbe kwenye kikao cha 19 taifa cha swala akisema kuwa ibada ya swala ni dhihirisho la mchanganyiko wa dunia na akhera na mfungamano wa mtu binafsi na jamii. Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa misikiti katika kila eneo na kitongoji inapaswa kuwa makimbilio ya amani, kheri na baraka, shule ya tafsiri ya Qur'ani na hadithi, minbari ya maarifa ya kijamii na kisiasa na kituo cha mawaidha na malezi ya maadili bora.

Ujumbe kamili wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ambao umesomwa leo na Hujjatul Islam Walmuslimin Raisi, Nabu wa Kwanza wa Mkuu wa Vyombo vya Sheria hapa nchini katika kikao cha taifa cha swala ni huu ufuatao:

Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehma, Mwenye kurehemu

Kuasisiwa mahala palipoitwa msikiti katika eneo la Quba kwanza na baadaye mjini Madina, ni miongoni mwa ubunifu bora na mzuri zaidi wa Uislamu katika kipindi cha mwanzoni mwa kuasisi jamii ya Kiislamu. Kuwa kwake nyumba ya Mwenyezi Mungu na nyumba ya wanadamu kwa wakati mmoja, mahala pa kwenda faragha na Mola na kukutana watu, kituo cha dhikri na ngazi ya kiroho, medani ya elimu, jihadi na mahala pa kufanyia tadbiri ya masuala ya kidunia na kituo cha siasa yote hayo yanaonyesha sura ya vitu viliyoshikamana na kuakisi sura ya msikiti wa Kiislamu na tofauti yake na maeneo ya ibada ya dini nyinginezo.

Shauku na raha ya ibada halisi katika msikiti wa Kiislamu imechanganyika na vuguvugu la maisha safi na yaliyojaa busara na humkurubisha mtu binafsi na jamii katika sura yake ya Kiislamu. Msikiti katika mtazamo na fikra za Kiislamu ni dhihirisho la mchanganyiko wa dunia na akhera na mfungamano wa mtu binafsi na jamii.

Kwa mtazamo huo, nyoyo zetu zinaenda dalki kwa ajili ya msikiti na kujawa na shauku na hisia za kuwajibika. Hii leo si wachache katika misikiti yetu watu wanaoweza kuonyesha taswira hiyo nzuri na ya kuvutia. Mahudhurio ya kizazi cha vijana wetu wenye maumbile safi wanazuoni na walimu werevu na wenye huruma misikitini yameifanya misikiti kuwa kituo cha dhikri, ibada, fikra na maarifa na kuzikumbusha nyoyo mambo yenye thamani kubwa. Hata hivyo hadi pale wajibu huo haujatekelezwa ipasavyo, hatupaswi wala hatuwezi kughafilika na hatari inayotishia jamii, vijana, familia na kizazi kijacho kutokana na uhaba wa misikiti au udhaifu na kutoshughulikiwa misikiti hiyo na kujinyima baraka kubwa zinazotolewa na misikiti ya Kiislamu kwa nchi, mfumo wa Kiislamu na wananchi.

Jambo la kwanza muhimu ni kujenga msikiti na kuwepo mwanazuoni anayestahiki katika msikiti huo. Licha ya kuwepo maelfu ya misikiti hapa nchini lakini bado tuna upungufu mkubwa wa maelfu ya misikiti vijijini, mijini, katika vitongoji na makazi ya watu. Ni haja ya dharura kwa waumini, vijana na mabarobaro kuweza kwenda misikitini kwa wepesi. Mwanazuoni mcha-Mungu, mwenye busara, mtaalamu na mwenye huruma na upendo katika msikiti mithili ya tabibu na muuguzi hospitalini, ni roho na uhai wa msikiti. Maimamu wa swala za jamaa wanapaswa kutambua kuwa ni wajibu wao kujitayarisha kwa ajili ya kutoa tiba ya kiroho na wanapaswa kusaidiwa na vituo vunavyoshughulikia masuala ya misikiti na vyuo vya kidini katika maeneo yote.

Msikiti unapaswa kuwa madrasa ya tafsiri ya Qur'ani na hadithi, minbari ya maarifa ya kijamii ya kisiasa na kituo cha mawaidha na malezi ya maadili mema. Chemchemi ya upendo wa wasimamizi, mudiri na viongozi wa misikiti inapaswa kuzivutia nyoyo za vijana na kuzitia shauku. Mahudhurio ya vijana katika misikiti yanapaswa kuhuisha na kuzidisha nishati na vuguvugu katika misikiti na kutia matumaini ya mustakbali mwema. Vilevile kunapaswa kuwapo ushirikiano mzuri kati ya misikiti na vituo vya elimu katika kila eneo. Itakuwa vyema mno kwa wanafunzi bora na walioshinda katika kila eneo kuhamasishwa na maimamu wa swala za jamaa misikitini na mbele ya macho ya wananchi. Msikiti unapaswa kuwa na uhusiano madhubuti na vijana wanaoana, watu wanaopata mafanikio ya kisayansi, kijamii, kisanaa na katika medani za michezo, watu wenye hima kubwa katika kusaidia wanadamu wenzo, watu wenye masaibu wanaotafuta njia ya utatuzi na hata watoto wanaozaliwa. Msikiti unapaswa kuwa makimbilio ya amani na sababu ya kheri na baraka na usiwe chanzo cha matatizo na maudhi kwa jirani wa msikiti huo.

Kurusha hewani sauti zinazoudhi watu hususan usiku na wakati wa mapumziko ya wananchi si jambo linalofaa na wakati mwingine huwa kinyume na sheria za dini. Sauti pekee inayopaswa kusikika kutoka misikitini ni sauti ya adhana inayotolea kwa sauti nzuri na ya kuvutia.

Kazi ya ujenzi wa misikiti na kuishughulikia ni wajibu wa wananchi wote na kila mtu anapaswa kushiriki katika suala hilo kulingana na hima na uwezo wake. Wananchi, mabaraza ya miji na taasisi za serikali kila kimoja kati ya vyombo hivyo kinapaswa kuwa na mchango katika kazi hiyo; wanazuoni hodari, wanaowajibika na wacha-Mungu wanaweza bali wanawajibika kuwa mhimili wa juhudi hizo takatifu.

Ninamuomba Mwenyezi Mungu atupe taufiki sisi sote na amzidishie umri, nishati na taufiki mwanazuoni mujahid na mchapakazi janabi Hujjatul Islam Walmuslimin Muhsin Qaraati.

Wassalam alaykum warahmatullah

Sayyid Ali Khamenei

18. Mehr 1389 (12/10/10)      

 

700 /