Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Taarifa ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu kuwashukuru wananchi wa Qum

Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mwishoni mwa safari ya siku kumi ya Ayatullah Ali Khamenei katika mji mtakatifu wa Qum imetoa shukrani za dhati kwa matabaka mbalimbali ya wananchi waumini, wenye maarifa na wakarimu na hamasa kubwa iliyoonyeshwa na wananchi wa Qum. Ofisi hiyo pia imewashukuru maraji', maulamaa na wanafunzi wa mji huo na kuelezea matumaini yake kwamba safari ya Kiongozi Muadhamu mjini humo itafungua ukurasa mpya katika historia iliyojaa fahari ya Qum.

Matini kamili ya ujumbe wa Ofisi ya Kiongozi Muadhamu ni hii ifuatayo:

Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehma, Mwenye kurehemu

"Leo waliokufuru wamekata tamaa katika dini yenu". (al Maidah: 3)

Qum, mbeba bendera ya harakati ya Kiislamu, kinara wa Mapinduzi ya Kiislamu na msaidizi wa siku zote na imara wa Uislamu na Imam Khomeini, imefanya mapokezi ya kihistoria ya kumkaribisha Kiongozi mwenye hikima wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuwathibitishia tena walimwengu kwamba Qum ilikuwa na itaendelea kuwa kituo kikuu na ngome ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Mandhari ya kuvutia na isiyoweza kusifika ya mapokezi ya matabaka mbalimbali ya wananchi wenye ikhlasi na mwamko wa mji wa jihadi kwa Ayatullah Ali Khamenei na mahaba yaliyoonyeshwa ya maraji', wanazuoni, wahadhiri na wanafunzi wa vyuo vya kidini vya mji huo kwa mara nyingine tena vimewaonyesha rafiki na adui kwamba muungano imara wa taifa na utawala wa faqihi ndio msingi wa heshima na adhama inayostawi kila siku ambayo Mwenyezi Mungu ameitunuku Iran azizi kwa baraka za imani, maarifa na kusimama kidete kwa kitaifa.

Hali iliyodhihiri katika siku za hivi karibuni katika mji mtakatifu wa Qum ambao ndio kituo kikubwa zaidi cha maarifa ya Ahlul Bait (as), imeonyesha kuwa njama mbalimbali zinazofanywa na madui wa Uislamu na Iran kwa ajili ya kutenganisha wananchi na Mapinduzi ya Kiislamu na kutenganisha dini na siasa hazikufua dafu na moyo na shuku kubwa ya kutetea Uislamu na Mapinduzi ya Kiislamu ambayo ndio kumbukumbu kubwa zaidi ya Imam Khomeini, bado inarindima katika nyoyo.

Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu inamshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu na kuwasilisha shukrani za dhati za kiongozi huyo kwa maraji', maulamaa, wanafunzi na matabaka yote ya wananchi wakarimu, wanamapinduzi na wenye maarifa wa Qum. Ofisi hiyo pia inamuomba Mola Karima auzidishie heshima na adhama mji wa Qum na kuimarisha zaidi Hauza na vyuo vya kidini vilivyobarikiwa na vya kihistoria vya mji huo mtakatifu.

Ni matarajio kwamba miongozo mbalimbali iliyotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mikutano yake na maulamaa, wahadhiri, viongozi wa Hauza ya Qum, wanafunzi wa vyuo vikuu, vijana, wanafunzi wa taaluma za dini, jeshi la kujitolea la Basiji, familia za mashahidi na vilema wa vita na kadhalika itakuwa mwanzo wa ukurasa mpya katika historia iliyojaa fahari ya Qum.

Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

8/ Aban/ 1389 (30/10/10)

     

700 /