Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu katika mkutano wa Mapambano ya Kimataifa dhidi ya Ugaidi:

Iran inalitambua suala la kupambana na ugaidi kuwa ni wajibu wake

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ametuma ujumbe kwenye mkutano wa Mapambano ya Dunia dhidi ya Ugaidi uliloanza leo mjini Tehran. Ayatullah Khemenei ameashiria katika ujumbe huo historia ya ugaidi wa madola makubwa ya kibeberu na uungaji mkono wao kwa tawala wa kigaidi na wa Kizayuni wa Israel na vilevile uovu wao mkubwa wa kusaidia kifedha na kipropaganda ugaidi unaofanyika kwa mpangilio maalumu huku yakidai kupambana na ugaidi na akasema: Moja kati ya kazi muhimu za mkutano wa sasa ni kuainisha maana ya wazi na halisi ya ugaidi. Ameongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalitambua suala la kupambana na uovu huo wa kishetani kuwa ni wajibu wake mkubwa na itaendeleza juhudi kwa nguvu zaidi katika njia ya mapambano hayo makubwa.

Ujumbe kamili wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni huu ufuatao:

Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehma, Mwenye kurehemu.

Wageni waheshimiwa na hadhirina muhtaramu! Ninakushukuruni kwa kukutana kwa ajili ya kuchunguza mojawapo na mambo yanayosababisha maafa kwa mwanadamu wa leo yaani ugaidi, na ninakukaribisheni hapa nchini Iran. Uchunguzi huu ambao bila shaka unapaswa kudumishwa na hatimaye kuwa azma na juhudi ya kweli ya jamii ya kimataifa, utafanikiwa kupiga hatua kubwa katika kukomesha ugaidi na kumwokoa mwanadamu kutokana na janga hilo la kuumiza. Sisi na kwa kutegemea uongozi na msaada wa Mwenyezi Mungu, tutaendeleza kazi hii kwa matumaini na kupiga hatua mbele kwa ushirikiano wa watu wote wenye nia njema na wanaohisi kuwajibika katika medani hii.

Ugaidi si jambo jipya wala matunda ya zama za hivi karibuni. Hata hivyo kujitokeza kwa silaha za kutisha na urahisi wa kutekelezwa mauaji yenye maafa makubwa dhidi ya halaiki ya watu vimelifanya jambo baya la ugaidi kuwa hatari na la kutisha zaidi na zaidi.

Nukta nyingine muhimu na ya kushtua ni kwamba mahesabu ya kishetani ya madola ya kibeberu ambayo yanatumia ugaidi kama wenzo wa kufikia malengo yao haramu, sasa yameingizwa katika siasa na mipango ya madola hayo.

Kumbukumbu za kihistoria za mataifa ya Mashariki ya Kati kamwe hazitasahau jinsi madola ya kikoloni yalivyoratibu makundi hatari ya kigaidi kama Wakala wa Kimataifa wa Uzayuni na makundi mengine zaidi ya kumi kama hilo na kutekeleza maafa ya Diir Yasin na kadhalika kwa shabaha ya kughusubu Palestina na kuwalazimisha wananchi madhlumu wa nchi hiyo kukimbia makazi yao.

Tangu kuundwa kwake hadi hii leo, utawala wa Kizayuni wa Israel umeendeleza waziwazi vitendo vyake vya kigaidi ndani na nje ya ardhi ya Palestina na kutangaza vitendo hivyo bila hata ya kuona aibu. Viongozi wa zamani na wa sasa wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamekuwa wakijifaharisha waziwazi kwa historia yao ya vitendo vya kigaidi na wakati mwingine kutangaza jinsi walivyoshiriki katika operesheni za mauaji ya kigaidi.

Mfano mwingine ni utawala wa Marekani ambao katika miongo ya hivi karibuni umekuwa na mwenendo mbaya sana wa kigaidi na kusaidia kifedha na kwa silaha ugaidi unaofanyika kwa mpangilio maalumu katika nchi za kanda hii. Mashambulizi angamizi ya ndege zisizokuwa na rubani dhidi ya familia zisizokuwa na ulinzi katika vijiji na maeneo yaliyobakia nyuma kimaendeleo katika nchi za Afghanistan na Pakistan, mashambulizi ambayo yamebadili sherehe zao za harusi na kuzifanya majlisi za maombolezo, jinai za Blackwater huko Iraq na mauaji yanayofanywa dhidi ya raia na wasomi wa nchi hiyo, misaada inayotolewa kwa makundi yanayolipua mabomu katika nchi za Iran, Iraq na Pakistan, mauaji ya wasomi wa nyuklia nchini Iran kwa kushirikiana na shirika la ujasusi la Israel Mossad, kutungua ndege ya abiria ya Iran katika anga ya Ghuba ya Uajemi na kuua karibu wasafiri 300 wakiwemo watoto, wanaume na wanawake.. ni sehemu ndogo tu ya maovu hayo ya kuaibisha ambayo kamwe hayatasahaulika. 

Marekani, Uingereza na baadhi ya nchi nyingine za Magharibi zenye faili jeusi na lilanowalaani la vitendo vya kigaidi, sasa zinadai kushika bendera ya mapambano dhidi ya ugaidi. Magaidi ambao katika mwongo wa 1980 walitekeleza mauaji ya kinyama dhidi ya maelfu ya watu ikiwa ni pamoja na mauaji ya kigaidi dhidi ya wasomi, wanasiasa na viongozi 72 wa ngazi za juu wa Iran katika tukio moja, na katika tukio jingine wakawaua shahidi rais na waziri mkuu wa wakati huo wa Iran, sasa wamepewa hifadhi na kuungwa mkono na madola na viongozi wa nchi za Ulaya.

Katika hali kama hiyo madai yao ya eti kupambana na ugaidi ni jambo la kufedhehesha.

Marekani na serikali za nchi za Ulaya sinazofuata kibubusa sera za Washington zinayapachika jina la magaidi makundi yanayoendesha mapambano kwa ajili ya kukomboa ardhi zao. Maana hii ya kupotosha ya ugaidi ni moja kati ya misingi mikuu ya tatizo la ugaidi katika dunia ya sasa.

 Katika mtazamo wa viongozi wa mfumo wa kibeberu, ugaidi una maana ya jambo lolote linalotishia maslahi yao haramu. Nchi hizo zinawaita wanamapambano wanaotumia haki yao ya kupambana na wavamizi kuwa ni magaidi, na wakati huo huo haziyatambui mapandikizi maovu na vibaraka wao ambao ni balaa kubwa kwa roho na usalama wa wananchi wasiokuwa na hatia kuwa ni magaidi.

Moja ya kazi muhimu za mkutano wenu wa sasa inaweza kuwa kuainisha maana ya wazi na kamili ya ugaidi.

Sisi, kwa kutegemea mafundisho ya Uislamu ambayo yanatambua utukufu wa mwanadamu kuwa ni moja ya vipaumbele vyake na yanayotambua kumuua mtu mmoja kuwa ni sawa na kuua wanadamu wote, na pia sisi kama taifa ambalo limepata hasara kubwa kutokana na ugadi katika kipindi chote cha miongo mitatu iliyopita, tunalitambua suala la kupambana na uovu huo wa kishetani kuwa ni wajibu unaopaswa kutekelezwa na tutaendeleza juhudi kwa nguvu zaidi katika njia ya mapambano hayo makubwa kwa uwezo na nguvu zake Mwenyezi Mungu.

Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yenu na juu ya waja wa Mwenyezi Mungu kote duniani.

Sayyid Ali Khamenei

3 Tir 1390 (25/06/11)

700 /