Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya Iran:

Taifa la Iran litayalazimisha kupiga magoti madola ya kibeberu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khameni mapema leo amewasili katika mji wa Bandar Abbas kusini mwa Iran na kukagua kiwanda cha Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu.

Baada ya kuwasili katika kambi ya jeshi la wanamaji wa Iran, Amiri Jeshi Mkuu alikwenda kwenye kumbukumbu ya mashahidi wa vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Saddam Hussein dhidi ya Iran na kuwakumbuka kwa kuwasomea dua na al Fatiha.

Baadaye Ayatullah Khamenei amekagua vikosi mbalimbali vya jeshi.

Ayatullah Khamenei amehutubia hadhara ya makamanda wa jeshi akiitaja bahari kuwa ni fursa kubwa ya kistratijia ya nchi na mataifa mbalimbali. Amesisitiza kuwa maslahi na suhula za bahari hizo ni mali ya mataifa na Jeshi la Wanamaji na Jeshi na Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) ni dhihirisho la uwezo wa taifa la Iran katika kulinda maslahi ya nchi hii katika eneo la Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman.

Amesema kuwa katika kipindi kirefu cha udhibiti wa tawala za kibeberu nchini Iran, tawala hizo zilizuia maendeleo na ustawi wa sekta ya jeshi la majini na kuwepo Iran katika maji ya kieneo na kimataifa, lakini leo hii Jeshi la Majini la Iran linapaswa kufanya jitihada maradufu kwa ajili ya kufidia kubakia nyuma kwa kipindi kirefu katika uwanja huo.

Akiashiria historia ya kuwepo majeshi ya madola ya kibeberu katika eneo nyeti mno la Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman, Ayatullah Khamenei amesema hali ya sasa inatofautiana na ya miaka iliyopita na pwani ndefu ya eneo hili sasa inadhibitiwa na nchi huru na taifa lenye fahari na lililoamka linalotambua vyema uwezo na azma yake ya kitaifa. Amesisitiza kuwa kwa msaada wake Allah, taifa hili litailazimisha nguvu yoyote ya kisiasa na kijeshi matakwa na irada yake na kuilazimisha kurudi nyuma.

Katika uwanja huo Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi yote ya Iran amesema leo hii eneo la Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman limekuwa eneo huru na linalojitawala kwa baraka za kuwepo Iran ya Kiislamu.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kuwepo majeshi ya majini ya Marekani na nchi za Ulaya katika eneo la Ghuba ya Uajemi kuna madhara na hakutakikani. Amesema kipindi ambacho madola ya kibebebru yalikuwa yakiyalazimisha matakwa yao kwa kupeleka majeshi yao katika maeneo mbalimbali kimepita. Amongeza kuwa hata kama kutakuwepo baadhi ya serikali katika eneo hili mbazo zinataka kufuata amri na imlaa ya madola ya kibeberu, lakini mataifa ya eneo hili yameamka na kuwa macho na yanakutambua kuwepo majeshi ya nchi hizo za kibeberu katika eneo hili kuwa kunavuruga amani na usalama.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa uwezo wa taifa hutayarisha uwanja mzuri wa kutumia baraka na manufaa ya bahari na akaongeza kuwa uwezo na nguvu hiyo inaweza kudhaminiwa na Jeshi la Wanamaji kwa kufanya jihadi na kujitolea.

Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya Iran amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijawahi kuihamasisha nchi yoyote ile kuingia katika vita na mapigano na itajitahidi kadiri ya uwezo kuepuka mpambano wa aina yoyote wa makusudi au sadfa. Hata hivyo amesisitiza kuwa nchi zinazoyaona maendeleo yao katika kutumia mabavu na dhulma zinapaswa kuelewa kwamba zinakabiliana na taifa imara na lenye nguvu.

Amelitaja Jeshi la Majini la Iran kuwa ni dhihirisho la nguvu na uwezo wa taifa. Ameliusia pia jeshi hilo kudumisha jihadi na bidii yake kwa ikhlasi na uwezo wake wote. Amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inajifaharisha kwa vijana wanaodhihirisha nguvu na uwezo wa taifa hili.

Ayatullah Ali Khamenei amezitaka asasi za serikali na viongozi mbalimbali kushirikiana na Jeshi la Majini.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja lengo la safari yake huko Bandari Abbas na kambi ya kijeshi ya eneo Nambari Moja la Kijeshi kuwa ni kuwatia moyo na kuwahamasisha zaidi wanamaji na jeshi lililoko katika eneo hilo. Amesema kuwa jihadi ya kimya kimya na yenye ikhlasi na moyo mkunjufu ya vijana wa taifa la Iran katika eneo hilo ni wema ambao utalipwa na Mwenyezi Mungu. 

Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Mkuu wa Jeshi la Majini la Iran Admeri Sayyari alitoa ripoti fupi akizungumzia nafasi ya bahari katika ustawi na maendeleo ya nchi mbalimbali. Amezungumzia pia maendeleo yaliyopatikana katika utengenezaji wa zana za kijeshi kama ukarabati wa meli za kivita, utoaji wa mafunzo, utumiaji wa askari wenye imani, ikhlasi na wataalamu na kushirikiana na vyuo vikuu na vituo vya elimu na sayansi.

Amiri Jeshi Mkuu pia amekagua vikosi vya nyambizi na meli za kivita, viwanda vya zana za kijeshi, na vituo vya mafunzo vya Jeshi la Majini.  
700 /