Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ayatullah Khamenei amesema katika ujumbe wa Hija:

Umma wa Kiislamu unahitajia kusimama kidete na kuwa macho mbele ya hila za ubeberu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ametoa ujumbe kwa mnasaba wa mkusanyiko mkubwa wa ibada ya Hija akiyataja mapambano na mapinduzi yaliyofanyika katika baadhi ya nchi za Kiislamu kuwa ni miongoni mwa masuala muhimu zaidi ya ulimwengu wa Kiislamu na kwamba hakika zilizomo katika harakati na mapinduzi hayo ni aya na alama za wazi za Mwenyezi Mungu. Ayatullah Khamenei ameashiria wajibu mkubwa wa kizazi kilichoamka cha vijana, wasomi na maulamaa wa kidini katika kipindi muhimu sana cha sasa na akasisitiza kuwa: "Umma wa Kiislamu hususan mataifa yaliyoanzisha mapambano yanahitajia mambo mawili kwa ajili ya kudumisha njia hiyo nayo ni 'kuendelea kusimama kidete' na 'kuwa macho mbele ya hila za madola ya kibeberu ya kimataifa'. Ameongeza kuwa nchi za Kiislamu haziwezi kuokoka na hatari inayozikabili bila ya kuwa na mshikamano, umoja na kuunda kambi madhubuti na yenye nguvu katika ulimwengu wa Kiislamu.

Matini kamili ya ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu ni hii ifuatayo:

Kwa Jina la Allah, Mwingi wa rehma, Mwenye kurehemu

Hamdu zote ni za Mola Mlezi wa viumbe na rehema Zake Allah na salamu Zake zimshukie Bwana wa wanaadamu wote, Muhammad al Mustafa, na Aali zake wema na Masahaba wake wateule.

Msimu wa machipuo wa Hija uliojaa usafi, uraufu na unyofu wa kimaanawi pamoja na utukufu na heshima kutoka kwa Mwenyezi Mungu umewadia, huku nyoyo za waumini wenye shauku kubwa zikizunguka Alkaaba ya tauhidi na umoja mithili ya vipepeo. Makka na Mina na Mash'ar na Arafa ni nyumbani kwa watu wenye bahati njema ambao wameitika mwito na mlingano wa Mwenyezi Mungu wa وَأَذِّن فِي النَّاسِ بِالْحَجِّ Na walinganie watu Hija... na wamepata fakhari ya kuingia kwenye ugeni wa Mwenyezi Mungu Mwingi wa maghufira, Mwingi wa ukarimu. Hapa ni katika ile Nyumba iliyobarikiwa (na Mwenyezi Mungu) na ni katika kitovu cha uongofu ambacho "Aya bainifu za Mwenyezi Mungu" zinang'ara ndani yake na kuwafunika kivuli cha amani watu wote walioko kwenye eneo hilo tukufu.

Zisafisheni nyoyo zenu kwa zamzamu ya unyofu, dhikri na unyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu na fungueni macho ya ndani ya nafsi zenu kwa ajili ya kuona Aya zilizo wazi za Mola wa Haki. Jipambeni kwa sifa za ikhlasi na kujisalimisha kikamilifu kwa Mwenyezi Mungu, jambo ambalo ni ishara ya uja na unyenyekevu wa kweli. Zifufueni na ziwekeni hai katika nyoyo zenu mara kwa mara, kumbukumbu za Yule baba (Nabii Ibrahim AS) ambaye kutokana na ikhlasi, unyenyekevu na kujisalimisha kwake kikamilifu kwa Mwenyezi Mungu, alimchukua Ismail wake na kumpeleka kwenye madhabahu (kwa ajili ya kumtoa kafara katika njia ya Mwenyezi Mungu). Ni kwa namna hiyo ndipo tutaweza kuijua njia ya wazi na inayong'aa ya kuweza kutufikisha kwa Mola Mlezi wetu, Mwingi wa utukufu. Piteni katika njia hiyo kwa hima ya imani thabiti na nia ya kweli-kweli.

Makamu ya Ibrahim ni moja ya ishara hizo bainifu za Mwenyezi Mungu. Mahali ulipo mguu wa Ibrahim AS pembeni mwa Alkaaba Tukufu ndiyo alama na nembo pekee ya Ibrahim. Mahala hapo alipokuwa akisimama (Nabii) Ibrahim (AS) ni mahala pa ikhlasi, kusamehe kila kitu na kujitolea kwake kikamilifu katika njia ya Mwenyezi Mungu, hapo palikuwa ni mahala kwa kuonyesha msimamo wake usiotetereka mbele ya matamanio ya nafsi na mapenzi ya baba kwa mwanawe na pia mbele ya nguvu za kufru na shirki na ubeberu wa Namrud wa zama zake.

Leo hii pia, mambo yote haya mawili yanamfungulia njia ya uongofu kila mmoja wetu katika umma wa Kiislamu. Hima, ushujaa na nia isiyotetereka ya kila mmoja wetu inaweza kutuongoza kwenye malengo yale yale ambayo Mitume wote wa Mwenyezi Mungu kuanzia Adam hadi Mtume wa Mwisho waliwalingania watu na kufanikiwa kuwaongoa baadhi yao kwenye saada na ufanisi wa duniani na Akhera.
Hii ni fursa nzuri na adhimu kwa umma wa Kiislamu na ni vyema kwa mahujaji kuzingatia masuala muhimu yanayohusiana na ulimwengu wa Kiislamu. Juu ya masuala yote hayo muhimu ya ulimwengu wa Kiislamu, kuna hii harakati ya mapinduzi katika baadhi ya nchi muhimu za Kiislamu. Baina ya msimu wa Hija wa mwaka jana na msimu wa Hija wa mwaka huu kuna matukio yametokea katika ulimwengu wa Kiislamu ambayo yanaweza kubadilisha kikamilifu mustakbali wa umma wa Kiislamu na yametoa bishara njema ya kupatikana mustakbali bora uliojaa heshima na mendeleo ya kimaada ya kimaanawi kwa Waislamu. Huko Misri, Tunisia na Libya, mataghuti, madikteta na watawala vibaraka na waharibifu wameng'olewa kwenye viti vya utawala, na katika baadhi ya nchi nyingine pia mawimbi makubwa ya mapambano ya wanachi yanatishia kuangamiza majengo ya kifakhari ya tawala za kitaghuti na kidikteta.
Ukurasa huu mpya uliofunguka katika historia ya umma wetu unabainisha uhakika ambao kila kipengee chake ni ishara bainifu za Mwenyezi Mungu ambazo zinatupa masomo na mazingatio makubwa katika maisha yetu. Uhakika huo inabidi utumike katika mahesabu yote ya mataifa ya Kiislamu.

Mosi ni kwamba hivi sasa katika kitovu cha mataifa ambayo kwa makumi ya miaka yalikuwa chini ya udhibiti wa kisiasa wa mabeberu wa kigeni kumezuka kizazi cha vijana ambao kwa kujipamba na sifa ya kupigiwa mfano ya kujiamini wamekubali kuingia kwenye hatari na kukabiliana na madola ya kibeberu na kutia hima ya kuleta mapinduzi na kubadilisha hali iliyopo.

Jengine ni kwamba licha ya watawala za kisekula kudhibiti kila kitu na kupambana na mafundisho ya dini kwa siri na kwa dhahiri katika nchi hizo, lakini wananchi wamejitokeza kwa wingi mno katika medani ya mapambano wakaziongoza vizuri nyoyo na ndimi zao; na mithili ya chemchemu zinazofoka, mamilioni ya watu wakaingia katika medani hiyo kwa maneno na matendo na kuipa uhai na utukufu mikusanyiko yao na matendo yao. Minara ya adhana, maeneo ya kusalia, takbiri, nara na kaulimbiu za Kiislamu; yote hayo ni ushahidi wa wazi wa uhakika huo, na kwamba uchaguzi wa hivi karibuni nchini Tunisia nao ni uthibitisho usio na chembe ya shaka wa ukweli wa jambo hilo. Ni kitu kisicho na shaka kwamba uchaguzi huru katika nchi yoyote nyingine ya Kiislamu hautakuwa na matokeo mengine ghairi ya kama yale yaliyotokea Tunisia (ya ushindi wa Waislamu katika uchaguzi huo).
Jengine ni kuwa, katika matukio ya mwaka huu mmoja uliopita, imewathibitikia watu wote kwamba, Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mwenye nguvu ametia nguvu katika azma na nia ya kweli ya mataifa ya wanaadamu kiasi kwamba, hakuna nguvu yoyote nyingine inayoweza kushinda nguvu hiyo ya wananchi. Wananchi wa taifa lolote lile wanaweza kubadilisha mustakbali wao kwa kutumia nguvu hiyo waliyopewa na Mwenyezi Mungu.

Jengine ni kwamba madola ya kibeberu yakiongozwa na Marekani, ambayo katika kipindi chote hiki cha makumi ya miaka wamekuwa wakizidhibiti mataifa ya Kiislamu kwa hila na mbinu mbali mbali kama za kisiasa na kiusalama, na kwa fikra zao, walidhani kuwa wamejifungulia jia kubwa lisilo na mpinzani yeyote kwa ajili ya kulidhibiti wanavyopenda eneo hili nyeti kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa, lakini hivi sasa madola hayo ya kibeberu yamekumbwa na mawimbi ya kwanza kabisa ya hasira na chuki za wananchi wa eneo hili. Inabidi kuwa na uhakika kwamba tawala zitakazoingia madarakani baada ya mapinduzi yanayoshuhudiwa katika mataifa ya Kiislamu, kamwe hazitakubaliana na milingano hiyo ya unyonyaji na ukandamizaji na kwamba jiografia ya kisiasa ya eneo hili itabadilishwa na wananchi kwa ajili ya kulinda heshima na uhuru wa mataifa ya eneo hili.
Jengine ni kuwa, tabia bandia na ya kinafiki ya madola ya Magharibi imezidi kufichuka mbele ya watu wa nchi za dunia. Nchi za Marekani na za Ulaya zilifanya juhudi zao zote kujaribu kuwalinda vibaraka wao katika nchi za Misri, Tunisia na Libya, lakini zilipoona haziwezi kupambana na maamuzi na nia thabiti ya wananchi, zilianza kuwachekea kinafiki wananchi wa nchi hizo na kujifanya ni marafiki wao.
Uhakika na ishara bainifu za Mwenyezi Mungu katika matukio ya mwaka mmoja uliopita katika eneo hili ni zaidi ya hayo ni si jambo zito kwa watu wenye mazingatio kuuona na kuutambua uhakika huo.
Lakini pamoja na hayo yote, leo hii umma mzima wa Kiislamu na hasa mataifa yaliyomo kwenye harakati za Mapinduzi, yanapaswa kuwa na mambo mawili makuu:

Mosi: Kuendelea na istikama na kusimama sawa sawa na kujiepusha vilivyo na kulegea azma na nia ya kweli iliyopo. Amri ya Mwenyezi Mungu iliyokuja katika Qur'ani Tukufu kwa Mtume Wake SAW ni kwamba: فَاسْتَقِمْ كَمَا أُمِرْتَ وَمَن تَابَ مَعَكَ yaani: "Basi, simama sawa sawa kama ulivyoamrishwa, wewe na wale wanaoelekea kwa Mwenyezi Mungu pamoja nawe." Pia Mwenyezi Mungu anasema: فَلِذَلِكَ فَادْعُ وَاسْتَقِمْ كَمَا أُمِرْتَ yaani: "Basi kwa haya waite! Nawe simama sawa sawa kama ulivyoamrishwa..."  Na vile vile kupitia kwa Nabii Musa AS Qur'ani Tukufu inasema:

 

قَالَ مُوسَى لِقَوْمِهِ اسْتَعِينُوا بِاللَّهِ وَاصْبِرُواْ إِنَّ الأَرْضَ لِلَّهِ يُورِثُهَا مَن يَشَاء مِنْ عِبَادِهِ وَالْعَاقِبَةُ لِلْمُتَّقِينَ

 

Yaani: "Musa akawaambia watu wake: Ombeni msaada kwa Mwenyezi Mungu, na subirini. Hakika ardhi ni ya Mwenyezi Mungu. Naye humrithisha amtakaye katika waja Wake. Na mwisho (mwema) ni wa wacha Mungu."

Dhihirisho kubwa la Taqwa hivi sasa kwa ajili ya mataifa yaliyosimama kwenye harakati ya mapinduzi ni kwamba wasisite wala kurudi nyuma katika harakati yao hiyo iliyojaa baraka na wala wasipumbazike na mafanikio waliyoyapata hadi sasa. Hii ni sehemu na hatua muhimu sana ya taqwa ambapo walio na taqwa hiyo huingia katika orodha ya wale watu ambao Mwenyezi Mungu amesema: "Na mwisho (mwema) ni wa wacha Mungu."

Pili: Ni kuwa macho na makini sana mbele ya hila za mabeberu wa kimataifa na madola ambayo yamepata pigo kutokana na harakati hizo za kimapinduzi. Mabeberu hawatakaa kimya, bali watatumia uwezo wao wote wa kisiasa, kiusalama na kifedha kupigania kurejesha ushawishi na nguvu zao katika nchi hizo. Silaha zinazotumiwa na mabeberu hao ni kutia tamaa, kutoa vitisho na kufanya hila na udanganyifu. Uzoefu mbali mbali unaonesha kuwa, wako baadhi ya shakhsia na watu muhimu katika jamii ambao hutekwa na silaha hizo na kuwafanya wamtumikie adui kwa kujua na kutojua kutokana na woga, tamaa na kughafilika. Jicho lililo macho la vijana, wasomi na maulamaa wa kidini linapaswa liwe makini mno katika suala hilo.
Hatari kubwa zaidi iliyopo ni uingiliaji na ushawishi wa kambi ya kufru na ubeberu katika mfumo mpya wa kisiasa wa nchi hizo. Maadui watafanya juhudi zao zote kujaribu kuzuia mifumo itakayokuja madarakani katika nchi hizo isiwe na sura ya Kiislamu na ya wananchi. Watu wote wenye uchungu na nchi hizo na wale wote wanaopigania heshima, utukufu na maendeleo ya nchi zao wanapaswa kufanya juhudi zao zote kuhakikisha kuwa mifumo mipya ya utawala itakayoingia madarakani katika nchi hizo inakuwa na sura ya Uislamu na ya wananchi. Katiba ina nafasi muhimu mno katika suala hilo. Kuweko umoja wa kitaifa, kutambuliwa rasmi makundi mengine ya kidini, kikabila na ya vizazi vingine ndilo litakalokuwa sharti la kupatikana ushindi mbali mbali katika siku za usoni.

Wananchi mashujaa na waliosimama imara na kufanya mapinduzi katika nchi za Misri, Tunisia, Libya na mataifa mengine yaliyoamka ya wananchi majasiri yanapaswa kujua kuwa njia pekee ya kuweza kuokoka na dhulma na kedi za Marekani na mabeberu wengine wa Magharibi ni kuimarisha nguvu zao na kuleta mlingano mzuri wa nguvu duniani kwa manufaa yao. Kama Waislamu wanataka kutatua masuala yao kwa njia bora mbele ya madola ya kibeberu ulimwenguni, basi wanapaswa kuifikia mipaka ya nadola makubwa duniani na hilo haliwezekani bila ya kuwepo ushirikiano, mapenzi, umoja na mshikamano kati ya nchi za Kiislamu. Na huo ndio wasia usiosahaulika aliotuachia Imam Khomeini (quddisa sirruh). Marekani na NATO kwa kisingizio cha kupambana na Gaddafi dikteta wamewashambulia kinyama wananchi wa Libya kwa miezi kadhaa. Gaddafi ni yule yule mtu ambaye kabla ya wananchi mashujaa wa Libya kusimama dhidi yake alikuwa rafiki wa karibu wa mabeberu na walikuwa wakimkumbatia na walikuwa wakipora utajiri wa Libya kupitia kwake kama ambavyo walikuwa wakimbusu mkono wake na wakisalimiana naye kwa shauku kubwa ili wapate kupora zaidi utajiri wa Libya, na baada ya wananchi kusimama dhidi yake, mabeberu hao hao wakamfanya Gaddafi kisingizio cha kuangamiza kikamilifu miundombinu yote ya Libya. Nchi gani duniani iliweza kuizuia NATO isifanye maafa na kuuawa watu kwa umati huko Libya? Kwa kweli kama meno na makucha ya madola makubwa hayatakatwa, basi hatari kama hizo zitaendelea kuzikabili nchi za Kiislamu na haiwezekani kujikomboa na uadui huo ila kwa kuundwa kambi yenye nguvu ya ulimwengu wa Kiislamu.

Leo hii Magharibi, Marekani na Uzayuni ni dhaifu zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Matatizo yao makubwa ya kiuchumi, kufeli kwao mtawalia huko Afghanistan na Iraq, upinzani mkubwa wa wananchi huko Marekani na katika nchi nyingine za Magharibi, upinzani ambao unaongezeka siku baada ya siku, mapambano na kuwa tayari wananchi wa Palestina na Lebanon kujitolea muhanga katika njia ya haki, mapambano ya kishujaa ya wananchi wa Yemen na Bahrain na katika nchi nyingine duniani zilizoko chini ya ushawishi na ubeberu wa Marekani, yote hayo yanabeba bishara kubwa nzuri kwa umma wa Kiislamu hususan nchi mpya za kimapinduzi. Wanaume na wanawake waumini katika kila kona ya ulimwengu wa Kiislamu na hasa hasa Misri, Tunisia na Libya wanapaswa kutumia kwa njia bora kabisa fursa hii iliyojitokeza ili kuunda kambi ya kimataifa ya Kiislamu yenye nguvu. Shakhsia muhimu na viongozi wa harakati za kimapinduzi wa nchi hizo wanapaswa kutawakali kwa Mwenyezi Mungu Mkubwa na kuwa na imani na ahadi ya nusra kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wanapaswa kuupambe ukurasa mpya uliofunguka katika historia ya umma wa Kiislamu kwa fakhari zitakazokumbukwa milele na ambazo zitakuwa ni chemchemu ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu na kuandaa uwanja wa kushuhudiwa nusura Yake.

Wassalaamu Alaa Ibadillahis Swalihin.

Sayyid Ali Husaini Khamenei

5/Aban/1390  

27 Mfunguo Pili Dhilqaad 1432.

 

 

700 /