Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Tutawaadhibu waliofanya jinai hiyo na washirika wao wa nyuma ya pazia

Kufuatia mauaji ya kigaidi yaliyofaywa dhidi ya msomi kijana Shahid Ahmadi Roshan, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ametoa ujumbe muhimu akisema kuwa, kinyume na njama zinazofanywa na kambi ya ubeberu, taifa kubwa la Iran litadumisha njia ya maendeleo kwa nguvu na azma kubwa zaidi. Amesisitiza kuwa Iran itawaadhibu waliofanya jinai hiyo na washirika wao wa nyuma ya pazia.

Matini ya ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni hii ifuatayo:

Kwa ajina la Allah, Mwingi wa rehma, Mwenye kurehemu.

Kuuawa shahidi msomi hodari na kijana Shahid Mustafa Ahmadi Roshan kumezitia huzuni na simanzi nyoyo za wapenzi wa elimu na wadau wa maendeleo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Sisi sote tunashirikiana na baba, mama, mke na mtoto wa kijana huyu madhlumu na hodari katika huzuni na majonzi yao.

Mauaji hayo ya kiwoga ambayo watekelezaji na wapangaji wake kamwe hawatakuwa na ujasiri wa kukiri jinai yao hiyo chafu na kubebeba lawama za kuhusika na kitendo hicho kiovu kama ilivyokuwa katika jinai nyingine zilizofanywa na kanali ya ugaidi wa kimataifa unaofanywa na serikali, yamepangwa au kufanyika kwa ushirikiano wa mashirika ya ujusisi ya CIA (la Marekani) na Mossad (la Israel), na ni ishara ya kufeli ubeberu wa kimataifa unaoongozwa na Marekani na Uzayuni katika njama zao za kukabiliana na taifa lililoazimia vilivyo, lenye imani na linalopiga hatua za maendeleo la Iran ya Kiislamu. Mabeberu hawa watashindwa pia katika mwenendo huu muovu na wa kikatili na hawatafikia malengo yao habithi na yaliyojaa shari.

Maendeleo yanayokwenda kwa kasi kubwa ya kielimu na mafanikio makubwa ya kisayansi yaliyopatikana hapa nchini kwa hima na azma kubwa ya vijana wenye imani, ghera na uwezo mkubwa kama Mustafa Ahmadi Roshan hayategemei mtu mmoja, bali ni harakati ya kihistoria inayotokana na azma kubwa ya kitaifa. Taifa la Iran litadumisha njia hiyo kwa nguvu na azma kubwa licha ya vinyongo vya viongozi wa kambi ya istikbari na mfumo wa ubeberu, na tutadhihirisha ustawi wa kuhusudiwa wa taifa kubwa la Iran kwa maadui wakubwa na mahasidi.  Vilevile tutawaadhibu waliofanya jinai hiyo na washirika wao wa nyuma ya pazia.

Ninatoa rambirambi na pongezi kwa wazazi, mke, mwana wa marehemu, jamii ya wanasayansi wa vyuo vikuu, na kwa ujumla wapenzi na wadau wa harakati ya elimu na sayansi hapa nchini kutokana na kuuawa shahidi Ahmadi Roshan na kuwatakia subira na uvumilivu. Vilevile ninamuomba Mwenyezi Mungu awape daraja za juu peponi mashahidi wetu wote na ninawakumbuka kwa kheri mashahidi Ali Muhammadi, Shahriyari na Rizaeinejad.

Sayyid Ali Khamenei

22/Dei/1390 (13/Januari 2012)           

700 /