Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ayatullah Khamenei:

Pato la mafuta linapaswa kuondolewa kabisa katika bajeti ya taifa

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema leo amekagua Kituo cha Utafiti wa Masuala ya Mafuta na kuona kwa karibu shughuli zinazofanyika katika kituo hicho. Ametaja shughuli na kazi za kituo hicho kuwa ni miongoni mwa fahari za taifa la Iran na huku akiashiria safari yake ya kukagua viwanda vya mafuta katika maeneo mbalimbali hapa nchini amesema mwaka huu wa 1390 Hijria Shamsia uliopewa jina la "Mwaka wa Jihadi ya Uchumi", unamalizika kama ulivyoanza kwa kukagua viwanda vya sekta ya mafuta na gesi, suala ambalo amesema, linaonesha umuhimu na taathira kubwa ya sekta hiyo katika harakati ya kiuchumi hapa nchini.  

Ayatullahil Udhmaa Ali Khamenei ameyasema hayo leo katika hadhara ya viongozi, wakurugenzi na wafanyakazi wa Kituo cha Utafiti wa Masuala ya Mafuta hapa nchini.

Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa kuna udharura wa kubadilishwa mtazamo wa taifa na viongozi wa nchi kuhusu suala la mafuta na kuongeza kuwa, kwa mujibu wa mipango ya ustawi wa taifa, mafuta yanapaswa kuondolewa kati ya vyanzo na fedha za bajeti ya taifa na kuwa chanzo cha kudhamini maendelea na ustawi wa kiuchumi wa Iran.

Amesema kazi na shughuli za kituo hicho ni miongoni mwa fahari za taifa la Iran. Ameongeza kuwa kutumia mapato ya mafuta kwa ajili ya kazi na shughuli za kila siku za taifa si jambo la busara na lina madhara makubwa.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa pato linalotokana na uuzaji mafuta katika hali ya sasa ndio nukta ya udhaifu wa nchi nyingi wazalishaji wa bidhaa hiyo. Ameongeza kuwa kwa nchi zinazouza mafuta yao kwa mujibu wa mahitaji na sera zinazopangwa na nchi za Magharibi na wakati huo huo hazifanyi jitihada za kupata elimu na sayansi ya kisasa huenda pato kama hilo likajaza mifuko ya watawala wao lakini halitakuwa na faida halisi, kwa sababu wakati mafuta hayo yatakapoisha nchi hizo zibakia nyuma na zisizokuwa na maendeleo.

Akifafanua fikra ya kuifanya sekta ya mafuta kuwa nguzo na nukta ya nguvu hapa nchini, Ayatullah Khamenei amesema kuna ulazima wa kufanyakazi kwa njia ambayo tutaweza kujichukulia maamuzi sisi wenyewe kuhusu kiwango za uzalishaji na uuzaji wa mafuta kwa mujibu wa maslahi yetu katika nyakati zote. Amesisitiza kuwa Iran imepata mafanikio makubwa katika njia hiyo na lengo hilo litafikiwa kikamilifu katika siku za usoni na Jamhuri ya Kiislamu itakuwa kigezo cha kuigwa na nchi nyingine katika uwanja huu.

Ayatullah Khamenei amepongeza kazi na jihadi kubwa inayofanywa na wasomi, watafiti, viongozi na wafanyakazi wa sekta ya mafuta na gesi hapa nchini na kusisitiza kuwa Iran inashika nafasi ya kwanza kwa kuwa na utajiri mkubwa wa mafuta na gesi na kwa msingi huo kuna udharura kwa wafanyakazi wa sekta hiyo kufikia kiwango cha juu kabisa cha elimu ya teknolojia na kushika nafasi ya kwanza.

Mwishoni mwa ziara hiyo ya kukagua Kituo cha Utafiti wa Masuala ya Mafuta na Gesi, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza kufurahishwa sana na matunda ya juhudi kubwa za wafanyakazi wa sekta ya mafuta na gesi na kusema kuwa ana matumaini kwamba juhudi za wafanyakazi wa sekta hiyo zitatayarisha uwanja mzuri wa kufikiwa malengo makubwa ya kitaifa.  

 

 

 

700 /