Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Uzalishaji wa Kitaifa, Kuunga Mkono Kazi na Rasilimali ya Kiirani”

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei leo ametoa ujumbe kwa taifa kwa mnasaba wa kuanza mwaka mpya wa 1391 Hijria Shamsia akitilia mkazo udharura wa kufanyika jihadi ya kiuchumi na kuwa na mahudhurio makubwa taifa la Iran katika nyanja mbalimbali za kiuchumi. Ameongeza kuwa sehemu muhimu ya jihadi ya kiuchumi inahusu suala la uzalishaji wa kitaifa na iwapo taifa litafanikiwa kutatua tatizo la uzalishaji wa ndani kwa kufanya hima, azma na kuwa macho sambamba na ratiba na mipango mizuri ya viongozi wa serikali, hapana shaka kwamba litashinda changamoto za adui.

Amewataka wadau wote wa masuala ya uchumi hapa nchini na taifa zima kufanya harakazi ya kustawisha uzalishaji wa ndani katika mwaka huu mpya na kuutaja uzalishaji wa kitaifa, kuunga mkono kazi na rasilimali za Kiirani kuwa ndio kaulimbiu ya mwaka huu wa 1391.

Matini kamili ya ujumbe wa mwaka mpya wa Kiongozi Muadhamu ni hii ifuatayo:

Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehma, Mwenye kurehemu

Ewe Mola unayebadilisha nyoyo na macho ya watu. Ewe Mola unayefanya tadbiri ya usiku na mchana. Ewe Mola ubadilishaye miaka na hali za waja. Badili hali zetu na uziweke katika hali bora zaidi.

Ewe Mola uliyetukuka! Kuwa walii, mlinzi, kiongozi, msaidizi, njia na jicho la Imam wa Zama Mahdi (as) na baba zake wakati wote, hadi utakapommakinisha katika ardhi na kumbakisha humo muda mrefu.

Mola Mlezi! Mpe Imam wa Zama yatakayomfurahisha katika nafsi yake, kizazi chake, Shia na wafuasi wake, raia wake, masahaba zake wa karibu, maadui zake na watu wote wa dunia.

Ninatoa mkono wa baraka na fanaka kwa wananchi kote nchini kwa mnasaba wa sikukuu ya Nowruz na kuanza mwaka mpya na pia kwa Wairani wote popote walipo duniani na kwa mataifa yote yanayosherehekea sikukuu ya Nowruz. Ninatoa mkono maalumu wa salamu za mwaka mpya kwa familia za mashahidi, walemavu wa vita na familia zao na wanaharakati wa nyanja mbalimbali. Ninamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu alipe taifa la Iranhali bora, nishati, ufanisi na furaha katika mwaka huu mpya na kubatilisha njama na malengo ya maadui wa taifa hili.

Mwaka uliopita wa 1390 Hijria Shamsia ulikuwa miongoni mwa miaka iliyokuwa na matukio mengi katika uga wa kieneo na kimataifa na hapa nchini. Jambo lililoshuhudiwa katika matukio hayo kwa ujumla ni kwamba yamekuwa na faida kwa taifa la Iran na kusaidia njia ya ukamilifu wa malengo yake. Watu wenye malengo na nia mbaya dhidi ya taifa la Iran, Iran na Uirani katika nchi za Magharibi wamekumbwa na matatizo mbalimbali.

Katika uga wa kieneo, mataifa ambayo yamekuwa yakiungwa mkono daima na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yamefikia malengo yao makuu, watawala wa kidikteta wameng’olewa madarakani, katiba zinazotegemea Uislamu zimepasishwa katika baadhi ya nchi hizo na adui nambari moja wa Umma wa Kiislamu na taifa la Iran yaani utawala wa Kizayuni wa Israel, amezingirwa.

Hapa nchini mwaka uliopita wa 1390 ulikuwa mwaka wa kudhihiri uwezo na nguvu ya taifa la Iran. Katika upande wa masuala ya kisiasa taifa la Iran lilikuwa na mahudhurio makubwa sana katika mwaka uliopita sawa katika maandamano ya kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapo tarehe 22 Bahman (11 Februari) au katika uchaguzi wa Bunge wa tarehe 2 Machi na limesajili vigezo vya uwezo wa kitaifa katika historia ya eneo hili ambavyo vilionekana kwa uchache mno katika miaka ya huko nyuma.

Katika mwaka uliopita taifa la Iranlimeweza kuhudhuria katika nyanja mbalimbali kwa nguvu zote na nishati kubwa na kuonesha utayarifu na uwezo wake mkubwa katika nyanja za kielimu, kijamii, kisiasa na kiuchumi licha ya uadui, propaganda chafu na hujuma za maadui wake.  Kwa baraka zake Mola, ulikuwa mwaka wenye mafaniko makubwa licha ya changamoto zilizojitokeza. Kama nilivyosema huko nyuma, hali ya mambo ilishabihiana na ile ya kipindi cha (vita vya) Badr na Khaybar, kwa maana ya hali ya kukubali changamoto na mashaka mbalimbali na kuyashinda.

Kama ilivyotangazwa mwanzoni mwa mwaka uliopita, mwaka 1390 ulikuwa Mwaka wa Jihadi ya Uchumi. Japokuwa weledi wa mambo walikuwa wakielewa kuwa jina, mwelekeo na kaulimbiu hiyo kwa ajili ya mwaka 1390 lilikuwa jambo la dharura, lakini  pia njama zilizofanywa na maadui hapo baadaye katika mwaka huo zilithibitisha tena udharura huo.

Tangu mwanzoni mwaka uliopita maadui wa Iranwalianzisha harakati ya kiadui katika medani ya uchumi dhidi ya taifa la Iran. Hata hivyo taifa la Iran, viongozi, matabaka yote ya wananchi na taasisi mbalimbali walikabiliana na vikwazo hivyo kwa tadbiri na uhodari na kufanikiwa kuzima athari za vikwazo hivyo kwa kiwango kikubwa. Mwaka 1390 ulikuwa mwaka wa harakati kubwa za kielimu, na Mungu akipenda katika siku zijazo nitalieleza taifa azizi la Iran baadhi ya maendeleo makubwa ya kisayansi na kiuchumi na juhudi mbalimbali zilizofanyika hapa nchini. Mwaka uliopita ulikuwa mwaka wa changamoto kubwa na harakati nyingi. Ulikuwa mwaka ambamo taifa la Iran liliweza kushinda changamoto mbalimbali.

Tunaanza mwaka mpya na kwa kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu, taifa la Iran sambamba na kufanya juhudi kubwa, harakati na kuwa macho, litaweza kupata tena mafanikio makubwa. Kwa mujibu wa maoni yangu na kwa kutilia maanani ripoti na ushauri wa wataalamu na weledi wa mambo, tumefikia natija kwamba changamoto kubwa zaidi katika mwaka huu unaoanza hivi sasa itakuwa katika medani ya uchumi. Jihadi ya uchumi si jambo linaloisha na kumalizika. Jihadi ya kiuchumi na jitihada kubwa za taifa la Irankatika nyanja za kiuchumi ni jambo lenye udharura mkubwa.

Mwaka huu ninayagawa masuala ya jihadi ya kiuchumi katika sehemu kadhaa. Sehemu moja ya masuala ya kiuchumi inahusu suala la uzalishaji wa ndani. Iwapo kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, azma kubwa ya taifa na juhudi za viongozi wa nchi tutaweza kustawisha uzalishaji wa ndani kamainavyostahiki, hapana shaka kuwa tutakuwa tumebatilisha sehemu kubwa ya njama za maadui. Hivyo basi, sehemu muhimu ya jihadi ya kiuchumi inahusu suala la uzalishaji wa kitaifa. Kama taifa la Iran litaweza kutatua tatizo la uzalishaji wa ndani na kupiga hatua katika uwanja huo kwa bidii, azma kubwa na maarifa pamoja na msaada wa viongozi na mipango sahihi, hapana shaka kuwa litashinda kikamilifu changamoto zilizopangwa na adui. Kwa msingi huo suala la uzalishaji wa kitaifa lina umuhimu mkubwa.

Kama tutaweza kustawisha uzalishaji wa ndani tutafanikiwa pia kutatua tatizo la mfumuko wa bei na suala la ajira na kuboresha zaidi uchumi wa ndani. Hali hii itamvunja moyo adui na kukomesha njama na uhasama wake.

Kwa msingi huo ninatoa wito kwa viongozi wote hapa nchini, wadau wa masuala ya uchumi na wananchi wote kuufanya mwaka huu kuwa mwaka wa ustawi wa uzalishaji wa ndani. Hivyo, kaulimbiu ya mwaka huu ni “Uzalishaji wa Kitaifa, Kuunga Mkono Kazi na Rasilimali ya Kiirani”.  Tunapaswa kuunga mkono kazi za mfanyakazi wa Kiirani na tulinde rasilimali za mwekezaji Muirani; na haya yatawezekana kwa kuimarisha zaidi uzalishaji wa ndani. Hisa ya serikali katika kazi hiyo ni kuhami uzalishaji wa ndani wa sekta za viwanda na kilimo. Mchango wa wenye rasilimali na wafanyakazi ni kuimarisha zaidi gurudumu la uzalishaji na umakini katika kazi ya uzalishaji. Mchango wa wananchi ambao katika mtazamo wangu ni muhimu zaidi ya yote, ni kutumia bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi. Tunapaswa kuwa na ada, tabia na utamaduni wa kutumia bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi. Tunapaswa kujiwajibisha kutumia bidhaa za ndani na kujiepusha kabisa na bidhaa zinazoingizwa nchini kutoka nje katika nyanja zote za matumizi wakati bidhaa kama hizo zinazalishwa hapa nchini.

Kwa msingi huo ni matarajio kwamba kwa mwelekeo huu taifa la Iran katika mwaka huu mpya wa 1391, litaweza kushinda njama na hila za maadui katika medani ya uchumi.

Ninamuomba Mwenyezi Mungu alipe taufiki taifa la Irankatika uwanja huu na nyanja zote. Namomba pia Allah amrehemu hayati Imam Khomeini na kuturudhia. Tunaziombea rehma na maghufira pia roho za mashahidi na awafufue na mawalii wao.

Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

   

700 /