Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya Iran:

Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ni jeshi la Mwenyezi Mungu na la Kiislamu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei

kabla ya adhuhuri ya leo (Jumapili) ametembelea kituo cha kikosi cha nchi kavu cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuona kwa karibu kazi na mafanikio ya kikosi hicho.

Ayatullah Khamenei ambaye ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametembelea pia eneo la makumbusho ya mashahidi wa vita vya kujihami kutakatifu na kuwasomea al Fatiha na dua mashahidi hao akimuomba Mwenyezi Mungu awapandishe daraja za juu za peponi.

Baada ya hapo, Ayatullah Khamenei amekagua maonyesho ya kazi za mafunzo, utafiti, uhandisi na masuala mbalimbali ya kijeshi ya kikosi cha nchi kavu cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ukiwemo mradi wa kushabihisha mafunzo ya kuruka na mwavuli uliobuniwa na watafiti na wasomi wa Kiirani na vilevile kuzungumza moja kwa moja kwa njia ya video na maafisa waliokuweko kwenye kambi ya Abu Dhar iliyoko kwenye eneo la SarPol-e-Zahab la mkoani Kermanshah magharibi mwa Iran na kundi la mstari wa mbele la kikosi cha nchi kavu cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kilichoko mkoani Zahedan (makao makuu ya mkoa wa Sistan na Baluchistan wa kusini mashariki mwa Iran).

Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Iran baadaye amewahutubia makamanda ya vitengo vya operesheni na masuala ya kijeshi vya kikosi cha nchi kavu cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu na akisisitiza juu ya mambo muhimu ya vikosi vya ulinzi na kuzingatia hima na misukumo inayotokana na imani za kidini amesema. Amesema katika kusimamia na kuendesha vikosi vya ulinzi, kuna udharura wa kupewe umuhimu mkubwa suala la kuimarishwa na kutiwa nguvu itikadi za kidini zinazobakia milele na kutoghafilika na jambo hilo wala kulizembea hata chembe kuhusu suala hilo.

Vilevile amesisitiza kwamba, kuwa na imani na Mwenyezi Mungu na kuwa na imani na mambo ya ghaibu kunaandaa kupatikana misukumo makini na yenye taathira kubwa na kuongeza kuwa, taathira za misukumo yenye kina kikubwa na ya kuweza kubakia milele ndani ya wanadamu waumini na mashujaa, inabainika katika nyakati nyeti na muhimu mno kama ilivyoshuhudiwa wakati wanamapambano wa Kiislamu na vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vilipoweza kupambana kiume na kukabiliana vilivyo na jeshi la Kibaath la utawala wa zamani wa Iraq lililokuwa limejiandaa vilivyo kwa silaha za kila namna huku likiungwa mkono na kusaidiwa na madola yote makubwa, na kulishinda.

Ayatullah Ali Khamenei amelitaja suala la kuuendeleza na kuutia nguvu moyo huo wa mapambano ndani ya vikosi vya ulinzi nchini Iran kuwa ni jambo la dharura na muhimu sana na kusisitiza kwa kusema: Makamanda wa jeshi nao wanapaswa sambamba na kujiimarisha kielimu na maarifa na ndani ya nafsi zao, wawe pia na moyo wa ikhlasi na kutopumbazika na kughururishwa na masuala ya kidunia.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amekitaja kikosi cha nchi kavu cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni sehemu muhimu na ya kimsingi ya jeshi hilo na amesisitiza juu ya haja ya kuweko mipango na ratiba nzuri za kukitia nguvu zaidi kikosi hicho na kuimarisha mafunzo yake.

Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu mbele ya makamanda wa vitengo mbalimbali vya operesheni vya kikosi cha nchi kavu cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu, Jenerali Ataullah Salehi, Mkuu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemkaribisha Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kutoa ripoti kuhusu kazi na maendeleo ya jeshi hilo.

Kwa upande wake, Brigedia Jenerali Ahmad Reza Pouristan, Kamanda wa Kikosi cha Nchi Kavu cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu naye ametoa ripoti kuhusu hali ya kikosi hicho na jinsi kilivyo tayari na imara wakati wote katika maeneo yote ya Iran kwa ajili ya kulilinda taifa.

Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ameendelea na hotuba yake mbele ya makamanda wateule, maafisa wenye vyeo jeshini, wanachuo na wafanyakazi wa kikosi cha nchi kavu cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu kwa kuashiria harakati inayozidi kukuwa na kuimarika ya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita na kusisitiza kuwa, leo hii Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni moja ya taasisi zenye sura ya kiraia kabisa kati ya taasisi za Iran na ni jeshi la Kiislamu linalozingatia sana mafundisho ya Mwenyezi Mungu na kwa hakika lipo kwa ajili ya kulitumikia taifa.

Ayatullah Khamenei vilevile ameashiria majigambo ya madola ya kibeberu yanayodai kuwa yameunda majeshi yao kwa misingi ya kulinda manufaa yao ya kitaifa na kuongeza kuwa, tofauti kabisa na yanavyodai madola ya kibeberu, majeshi ya madola hayo yanatumikia tu jaha na uluwa wa kisiasa na kuyalinda madola ya kitaghuti na kwamba hayayapi umuhimu wowote manufaa ya raia wa nchi zao.

Amehoji kwa kusema, vipi jeshi la Marekani litadai kuwa linalinda maslahi ya raia na watu wa Marekani wakati linaua raia huko Iraq na Afghanistan na kufanya jinai nyingine nyingi katika nchi hizo?

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndilo jeshi pekee linalotumikia vilivyo wananchi na kulinda manufaa ya taifa lake na kwamba itikadi na hisia za jeshi hilo na za makamanda wa jeshi hilo nazo ni sawa sawa kabisa na hisia na itikadi za wananchi.

Ayatullah Khamenei amekutaja kuundika kwa jeshi kama hili la Iran kuwa ni matunda ya harakati inayozidi kukuwa na kuimarika ya jeshi hilo baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kuongeza kuwa: Inabidi harakati hiyo iliyojaa baraka izidi na kupata nguvu siku baada ya siku katika jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Akibainisha nafasi ya Jeshi la Mfumo wa Kiislamu amesema: Hivi sasa duniani kumeundika mrengo ambao unapinga mgawanyo wa nchi kati ya zile za kibeberu na zile zinazopasa kufanyiwa ubeberu ambapo kitovu cha mrengo huo ni Iran ya Kiislamu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja sababu kuu ya kushuhudiwa vitisho, kusakamwa taifa la Iran pamoja na vikwazo vya maadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kwamba ni kutokana na Iran kuwa kitovu na kituo kikuu cha harakati hiyo na kusisitiza kuwa, baada ya kupita zaidi ya miongo mitatu, harakati hiyo muhimu mno imezidi kujikita na kuimarika katika nyoyo za mataifa ya Waislamu na hivi sasa imekuwa ni nguvu imara sana ambapo matukio ya Misri na katika baadhi nyingine ya nchi za Kiislamu ni matunda ya jambo hilo.

Ayatullah Khamenei amegusia pia woga mkubwa walio nao wakoloni na kambi ya kibeberu kuhusiana na mrengo na harakati hiyo inayozidi kuimarika na kuongeza akisema kuwa, sababu ya madola hayo ya kikoloni na kiya beberu kuwa na woga wote huo ni vijana wa Iran ya Kiislamu wenye nia thabiti na imani imara na tabasuri, muono wa mbali na maarifa mazuri ya wananchi wa Iran sambamba na hisia zao za kitaifa mambo ambayo yameimarika mno hivi sasa nchini Iran na kupelekea kuzidi kupata nguvu harakati hiyo katika kitovu cha mrengo huu, yaani Iran.

Ameongeza kuwa, Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ni sehemu muhimu na nyeti sana katika majimui hiyo na kwamba jeshi hilo linatakiwa liweko imara na tayari tayari kikweli kweli, wakati wote.

         

700 /