Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Amiri Jeshi Mkuu atembelea maonyesho ya kazi za jeshi

Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Ali Khamenei leo asubuhi (Jumanne) ametembelea maonyesho ya kazi na mafanikio ya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu na kuona kwa karibu mwenendo wa kazi na maendeleo ya kiufundi, kiulinzi, kijeshi na kielimu wa sekta mbalimbali za jeshi hilo mjini Nowshahr, kaskazini mwa Iran.

Mwanzoni mwa kutembelea maonyesho hayo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amepatiwa ripoti kuhusu namna kilivyoundwa Kikosi cha Kaskazini cha Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na jinsi kinavyofanya kazi kwa umakini wa hali ya juu katika kulinda usalama wa eneo lililoko kwenye mipaka ya kikosi hicho.

Mfumo wa kikosi hicho wa kukusanya taarifa na mawasiliano pamoja na kukiweka mbali kituo cha kikosi hicho na vyanzo vya mionzi ni miongoni mwa vitu vilivyokuwemo kwenye maonyesho hayo na ni moja ya viungo vya asili vya Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu katika mipaka ya majini iliyoko chini ya udhibiti wa Iran kwenye bahari ya Caspian.

Katika sehemu hiyo, Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Ali Khamenei amewasiliana moja kwa moja na kamanda wa kikosi cha 22 cha Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu kilichotumwa kikazi katika Bahari ya Hindi, kwenye lango la Babul Mandab na Bahari Nyekundu na kumuomba Mwenyezi Mungu awape taufiki wale wote wanaolinda heshima na utukufu wa taifa la Iran.

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Elimu za Baharini cha Imam Khomeini huko Nowshahr, kaskazini mwa Iran nao wameonyesha sehemu ya kazi zao katika maonyesho hayo.

Kuongezwa mfumo wa mionzi ya leza ndani ya ndege zisizo na rubani ili kuongeza umakini wa kugundua na kupiga shabaha na kugundua vyombo vinavyokwepa kuonekana na rada vya chini ya maji, kuendesha mitambo kutokea mbali kama vile mfumo uliopewa jina la "Taha" n.k, ni miongoni mwa kazi zilizoonyeshwa kwenye maonyesho hayo. "Taha" ni mfumo unaotumia mawimbi ya sauti kwa ajili ya kudhibiti na kuongoza vyombo kwa kutokea mbali.

Mfumo wa kurushia kombora la "Jask 2" ambalo lina uwezo wa kufungwa juu ya vyombo vya chini ya maji na kufyatuliwa kuelekea kwenye shabaha inayokusudiwa ni miongoni mwa maendeleo ya kielimu ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Elimu za Baharini cha Imam Khomeini huko Nowshahr, yaliyoonyeshwa kwenye maonyesho hayo. Kombora hilo limebuniwa na kutengenezwa kwa pamoja na Wizara ya Ulinzi, Taasisi ya Jihadi ya Kujitosheleza ya Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na vituo mbalimbali vya Vyuo Vikuu nchini.

Vyuo vikuu vya maafisa wa kijeshi wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ikiwa ni pamoja na Chuo Kikuu cha Maafisa wa Kijeshi cha Imam Ali AS, Chuo Kikuu cha Khatamul Anbiyaa - Chuo Kikuu cha Shahid Sattari - na Chuo Kikuu cha Elimu za Tiba cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran navyo vimeonyesha miradi yao kadhaa ya utafiti na utekelezaji wa kivitendo  katika maonyesho hayo. Kubuni na kutengeneza rada mbili za kisasa kabisa za Samen na Shahab kwa kushirikiana na vituo mbalimbali vya kielimu nchini ni miongoni mwa miradi hiyo.

Katika sehemu ya maonyesho ya kazi na matunda ya kikosi cha majini, kumetolewa ripoti kuhusu kazi za kielimu na kivitendo zilizofanyika kwa ajili ya kutia nguvu uwezo wa baharini, utengenezaji wa vyombo vya kisasa vya juu na chini ya maji, masomo yanayotolewa na kasi mwenendo wa kujitosheleza kikosi hicho.

Jinsi ya kuweko mfumo wa kusimamia elimu na utengenezaji wa filamu za matukio ya kweli kuhusiana na kazi na maendeleo mbalimbali ukiwa ni msingi wa ufundishaji na usambazaji wa elimu ya mafanikio hayo ni miongoni mwa masuala ambayo ameonyeshwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwenye sehemu hiyo ya maonyesho.

Katika sehemu hiyo pia pametolewa ripoti kuhusu jinsi kikosi cha majini kinavyojitosheleza katika ukarabati wa vyombo mbalimbali vizito na vyepesi ikiwemo nyambizi nzito aina ya Tariq. Tariq ni miongoni mwa teknolojia tata na nzito sana zilizoko duniani leo. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kumetumika vipande laki mbili vyilivyokarabatiwa na karibu vipande 50 vilivyotengenezwa upya kabisa katika kazi ya kukarabati nyambizi hiyo ya kisasa.

Kukata utegemezi wa nje na kuifanya elimu kuwa ya ndani ya Iran kikamilifu ni miongoni mwa malengo makuu ya mradi huo mkubwa.

Katika sehemu hiyo, Luteni Kanali Husain Hariri, Kamanda wa kikosi cha vyombo vya chini ya maji cha Divisheni ya Kwanza ya Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu sehemu ya kusini mwa Iran amewasiliana moja kwa moja na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kutangaza kuweko imara na tayari kikamilifu nyambizi ya Tariq kwa ajili ya kutekeleza wajibu na amri yoyote kutoka kwa Amiri Jeshi Mkuu, Ayatullah Udhma Ali Khamenei. Vilevile katika sehemu hiyo ya maonyesho, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameonyeshwa filamu ya jinsi inavyoendelea kazi ya kuandaa na kutengeneza manowari aina ya Sahand ya kufanyia kazi kadhaa ambayo hivi sasa imo katika hatua za kutengenezwa na pia manowari ya makombora ya Pekyan ambayo nayo imo katika hatua za matengenezo.

Kepteni Jafar Saidi, Kamanda wa Viwanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko Bandar Abbas katika mawasiliano ya moja kwa moja amemuomba Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Iran, Ayatullah Ali Khamenei, atoe idhini ya kushushwa majini sehemu ya asili ya manowari ya Sahand. Sekunde chache baadaye sehemu hiyo muhimu na ya asili ya manowari ya Sahand imeshushwa majini kwa idhini ya Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Katika muda wote wa kutembelea maonyesho hayo, Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Iran alikuwa anapewa maelezo na ufafanuzi na makamanda na maafisa husika wa miradi yote muhimu. Miongoni mwa miradi hiyo ni ule wa kutengeneza manowari ya mafunzo na ya kufanyia operesheni za Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kubuniwa mradi huo ni hatua muhimu sana katika kuongeza umakini na kuyapa uzito zaidi mafunzo ya maafisa wa daraja na vyeo mbalimbali wa jeshi hilo. Baada ya kubuniwa mradi huo, hatua itakayofuatia ni kutengenezwa manowari ya kwanza kabisa ya kazi hiyo katika jeshi hilo.

Matunda mengine ya kazi za Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu yaliyoonyeshwa katika maonyesho hayo ni ulinzi wa mipaka ya majini ya Iran kwa kutumia mawasiliano ya kompyuta ikiwa ni pamoja na namna ya kukabiliana na kuvunja mashambulizi na vitisho vya maadui kupitia mawasiliano ya kompyuta.

Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametembelea maonyesha hayo kwa muda wa masaa mawili na katika sehemu inayohusiana na mapambano kupitia mawasiliano ya kompyuta, wataalamu wa Iran wametoa ufafanuzi juu ya jinsi wanavyofanya kazi zao.

 

 

700 /