Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Taifa la Iran halijawahi kumchokozi yeyote lakini halitanyamazia kimya uchokozi wa aina yoyote

Mapema leo Ayatullah Ali Khamenei ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi yote ya Iran amekagua gwaride la vikosi vya jeshi na jeshi la kujitolea na Basij katika mkoa wa Khorasani Kaskazini katika kambi ya Shahid Nuri ya Kikosi cha nchi kavu cha Jawadul Aimma cha jeshi la Sepah huko Bojnurd.

Baada ya kuwasili katika kambi hiyo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alikwenda moja kwa moja kwenye makaburi ya kumbukumbu ya mashahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuwasomea al Fatiha sambamba na kuwaombea dua mashahidi hao.

Baadaye Ayatullah Khamenei ametoa hotuba mbele ya vikosi vya Jeshi la Ulinzi akilitaja jeshi hilo kuwa ni nguzo ya usalama wa taifa na mlinzi wa nchi mbele ya hujuma za wageni. Amesema kuwa, taifa linalofuata mafundisho ya Uislamu la Iran halitaanzisha mashambulizi dhidi ya upande wowote lakini halitanyamaza kimya mbele ya shambulizi la aina yoyote.

Amebainisha kuwa lengo la kuchochea vita la mabeberu ni kupata fursa ya kuuza silaha na kustawisha viwanda vya kutengeneza silaha vya mabepari na kuongeza kuwa, suala pekee linalodhoofisha nia ya kuchochea vita ya mabeberu hao au kuondoa kabisa nia hiyo ni kujiweka tayari kikamilifu kwa taifa na kuwa tayari vikosi vya jeshi (kwa ajili ya kukabiliana na mabeberu hao).

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, utayarifu wa taifa la Iran hususan tabaka la vijana kwa ajili ya kukabiliana na mabeberu unahisika zaidi sasa kuliko wakati wowote mwingine na vikosi vya Jeshi la Ulinzi vimejitayarisha zaidi kuliko ilivyokuwa huko nyuma.

Ayatullah Ali Khamenei amesema, kumkumbuka Mwenyezi Mungu na masuala ya kiroho ndio sababu kuu ya kuzidishiwa nguvu na uwezo wa kujilinda wa vikosi vya Jeshi la Ulinzi. Ameongeza kuwa, ushindi wa jeshi la Iran ya Kiislamu katika vita vya miaka minane ya Kujitetea Kutakatifu na kushindwa jeshi lililojizatiti kwa silaha na lenye majigambo la utawala ghasibu wa Israel katika vita vya siku 33 huko Lebanon na siku 22 katika Ukanda wa Gaza ni mfano bora zaidi wa taathira ya masuala ya kiroho katika kuzidisha uwezo na nguvu za kujilinda.

Amesema kuwa hii leo taifa la Iran linahisi kuwa na nguvu kubwa zaidi kuliko wakati wowote mwingine na hisia hiyo inategemea ukweli wa mambo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza juu ya udharura wa kulindwa na kuimarishwa nguvu na utayarifu wa taifa na jeshi la Iran na kusema kuwa, utayarifu na uchapakazi wa taifa la Iran na jeshi lake vimeipa nchi hii heshima na haiba kubwa kiasi kwamba haiwaruhusu maadui hata kufikiria tu suala la kuishambulia Iran.

Kabla ya hotuba ya Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya Iran, Brigedia Jenerali Ja’fari ambaye ni Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) alitoa hotuba fupi akiashiria uwezo mkubwa wa jeshi hususan Sepah na kusema kuwa, mbali na kufuatilia kwa karibu vitisho vya adui, jeshi hilo limezidisha utayarifu wake na kuzidisha uwezo wa kujilinda, masafa ya makombora yake na uwezo wa vikosi vyake vya majini.          

   

700 /