Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Katika Mtazamo wa Imam Khomeini

Masharti ya Uongozi

Masharti Mawili Makuu

Masharti ya dharura ya uongozi yanatokana moja kwa moja na muundo wa serikali ya Kiislamu. Baada ya masharti ya kimsingi kama vile kuwa na akili timamu na tadbiri, kuna masharti mawili makuu yanayopaswa kuzingatiwa katika kiongozi wa dola la Kiislamu ambayo ni:
1- Utambuzi wa sheria
2- Uadilifu.
Japokuwa baada ya kufariki Mtume Mtukufu (saw) kulitokea hitilafu juu ya nani anapaswa kuwa khalifa wake, lakini Waislamu hawakuhitilafiana juu ya ukweli kwamba khalifa na kiongozi wa baada ya Mtume anapaswa kuwa mtu bora zaidi. Hitilafu zao zilikuwa kuhusu maudhui mbili.
1- Kwa kuwa serikali ya Kiislamu ni serikali ya sheria ni lazima kwa mtawala awe na elimu na ujuzi wa sheria kama ilivyopokelewa katika hadithi. Si kwa mtawala pekee, bali kila mtu anapaswa kuwa na ujuzi wa sheria kuhusu kazi, wadhifa na cheo anachokuwa nacho. Hata hivyo mtawala anapaswa kuwa mjuzi na mwenye elimu zaidi. Maimamu kutoka katika Nyumba Tukufu ya Mtume walithibitisha kwa dalili uimamu wao kwa hoja kwamba Imam anapaswa kuwa bora zaidi ya watu wengine. Maulamaa wa Kishia pia wametoa hoja kwa maulamaa wa madhehebu nyingine kwamba khalifa aliyeshindwa kujibu swali la kisheria hastahiki kuwa imamu na kiongozi wa Waislamu baada ya Mtume (saw). Khalifa aliyetenda amali fulani kinyume cha sheria za Kiislamu hastahiki kuwa imamu…(1)
Maarifa ya sheria na uadilifu katika mtazamo wa Waislamu ni sharti na nguzo muhimu. Masuala mengine hayaingilii wala hayana udharura katika suala la uimamu. Kwa mfano elimu kuhusu Malaika, na utambuzi wa sifa za Mola Muumba haviingiliani na suala la uimamu. Kama ambavyo anayejua elimu zote za sayansi asilia (bayolojia, kemia na fizikia) na kuvumbua nguvu zote za maumbile, au mtaalamu wa muziki hastahiki kuwa khalifa wala haweza kutangulizwa mbele ya mtambuzi wa sheria za Kiislamu na muadilifu kwa ajili ya kuongoza serikali.
Suala linaluhusiana na ukhalifa (uongozi wa Waislamu baada ya Mtume saw) na ambalo lilijadiliwa na kuzungumziwa katika zama za Mtume Muhammad (saw) na Maimamu wetu (as) na halikutiliwa shaka baina ya Waislamu ni kuwa, awali mtawala na khalifa anapaswa kuwa mjuzi wa sheria za Kiislamu, yaani mtaalamu wa sheria. Pili anapaswa kuwa muadilifu na mkamilifu katika itikadi na masuala ya kimaadili. Akili ya mwanadamu pia inahukumu hivyo, kwani serikali ya Kiislamu ni serikali ya sheria na kanuni na si ya kidhalimu au utawala wa watu juu ya watu wengine.
Iwapo mtawala hajui masuala ya sheria hastahiki kutawala; kwani kama atakalidi, basi serikali itapoteza uwezo na haiba yake, na iwapo hatakalidi hawezi kuwa mtawala na mtekelezaji wa sheria za Kiislamu. Vilevile imethibiti kwamba "wanazuoni wa fiqhi ni wakuu wa watawala"(2) (kwa maana kwamba watawala Waislamu wanapaswa kuwafuata wanazuoni wa fiqhi na kuwauliza sheria na kisha kuzitekeleza. Wakati huo watawala halisi watakuwa ni wanazuoni wa fiqhi na sheria za Kiislamu. Hivyo basi, mamlaka yanapaswa kushikwa rasmi na wasomi wa fiqhi na si watu ambao wanalazimika kuwafuata wasomi hao kwa sababu ya kutojua sheria.
2- Mtawala anapasa kuwa mkamilifu katika upande wa itikadi na maadili na kuwa muadilifu. Hapasi kuwa mtu aliyechafuliwa na maasi. Mtu anayetaka kutekeleza sheria za adhabu za Uislamu, kusimamia hazina ya Waislamu na matumizi ya serikali ambaye Mwenyezi Mungu amempa mamlaka ya kuendesha mambo ya waja wake, anapasa kuwa mtu asiyefanya maasi kama inavyosema Qur'ani Tukufu: "Akasema (Mwenyezi Mungu): Ahadi yangu haitawafikia madhalimu."(3) Mwenyezi Mungu Mtukufu kamwe hampi mamlaka mtu wa aina hiyo.
Mtawala anapokosa sifa ya uadilifu hatatenda uadilifu katika kutoa haki za Waislamu, kukusanya ushuru na kuutumia kwa njia sahihi na katika kutekeleza sheria za adhabu za Kiislamu. Aidha yumkini akaitwisha jamii wasaidizi, wafuasi na jamaa zake na kutumia hazina ya dola katika malengo na matamanio yake ya kinafsi.(4)
Kuwa marja' si sharti la lazima
Tokea awali nilikuwa nikiamini na kusisitiza kwamba kuwa marja' si sharti la mtu kuwa kiongozi wa serikali ya Kiislamu. Inatosha kuwa mujtahid (mtu mwenye uwezo wa kielimu wa kunyambua sheria za fiqhi ya Kiislamu) muadilifu aliyepasishwa na Baraza la Wataalamu wa kumchagua kiongozi (Khobregan) kutoka maeneo yote nchini. Iwapo wananchi watawachagua wataalamu hao ili wamuainishe mujtahid muadilifu wa kuongoza serikali yao basi mtu yeyote atakayeainishwa na wataalamu hao kuchukua uongozi, atakuwa amekubaliwa na wananchi. Katika sura hiyo atakuwa kiongozi aliyechaguliwa na wananchi na amri zake zinakuwa lazima kutekelezwa.(5)
Kigezo cha uongozi
Katika zama za awali za Uislamu kulitokea serikali mbili halisi za Kiislamu katika vipindi viwili tofauti. Kwanza ni katika kipindi cha Mtume (saw) na pili ni wakati wa utawala wa Imam Ali bin Abi Twalib (as) huko Kufa, Iraq. Katika vipindi hivyo viwili thamani za kiroho zilitawala. Kwa maana kwamba kulisimamishwa serikali ya kiadilifu ambapo mtawala hakukiuka sheria hata kidogo. Serikali ya vipindi hivyo viwili ilikuwa serikali ya sheria na huenda hakujawahi kushuhudiwa tena utawala wa sheria kama huo katika kipindi kiingine chochote. Ilikuwa serikali ambayo kiongozi wake (kwa sasa anaitwa Rais wa Jamhuri au Sultani) alikuwa sawa na mtu wa chini kabisa katika eneo hilo mbele ya sheria. Hali hiyo ilionekana katika zama za awali za Uislamu. Historia imenukuu kisa kama hicho cha Amirul Muuminin Ali bi Abi Twalib. Wakati mtukufu huyo aliposhika mamlaka na kutawala eneo lililoanzia Hijazi hadi Misri, Iran na maeneo mengine mengi na makadhi walikuwa wakiteuliwa na yeye mwenyewe, kulitokea kesi ya madai kati ya Imam Ali na mtu mmoja kutoka Yemen iliyokuwa chini ya mamlaka yake. Kadhi alimwita Amirul Muuminin mahakamani. Wakati Imam Ali (as) alipoingia mahakamani kadhi alitaka kuinuka na kumpa heshima (kama kiongozi mku wa serikali). Imam alisema: Katika kukata kesi usimpe heshima maalumu mtu mmoja (kati ya wawili wanaoshtakiana). Mimi na yeye (mdai) tunapasa kuwa katika daraja sawa. Kadhi alikata kesi dhidi ya Amirul Muumini na kumpa haki raia Myemen. Imam Ali (as) aliondoka mahala hapo akiwa ameridhika.
Hiyo ndiyo serikali ambayo watu wote huwa sawa mbele ya sheria. Kwani sheria ya Uislamu ni sheria ya Mwenyezi Mungu na watu wote ni sawa mbele Yake sawa awe mtawala au raia, Mtume au Imam, au mtu mwingine yeyote.(6)
Nafasi ya kiongozi baina ya wananchi
Mtawala na kiongozi wa Kiislamu si kama watawala wengine mithili ya masultani au maraisi wa jamhuri. Kiongozi wa Kiislamu ni kiongozi ambaye alikuwa akienda katika msikiti wa Madina pamoja na watu wengine na kusikiliza maneno yao. Wale wote waliokuwa na madaraka walikuwa wakikusanyika msikitini kama watu wa matabaka mengine. Walikusanyika kwa namna ambayo mgeni kutoka nje hakuweza kutofautisha baina ya rais wa dola, viongozi wenye nyadhifa mbalimbali na raia wa kawaida. Nguo zake zilikuwa sawa na za raia wa kawaida na maingiliano yake na watu yalikuwa kama ya watu wengine. Uadilifu ulitekelezwa kiasi kwamba iwapo raia wa chini kabisa atawasilisha kesi mahakamani dhidi ya kiongozi mkuu wa serikali, kadhi alimwita mahakamani kiongozi huyo naye aliitikia wito huo.(7)
Utawala wa Faqihi unapinga udikteta
Katika Uislamu sheria ndiyo inayotawala. Mtume Mtukufu (saw) pia alikuwa akifuata sheria za Mwenyezi Mungu na hakukika sheria hizo. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema, iwapo utasema lolote tofauti na niyasemayo mimi, nitakuadhibu na kukata mshipa wako mkubwa wa moyo.(8) Iwapo Mtume (saw) angekuwa dikteta na kiongozi ambaye watu wangeogopa asifanye udikteta kutokana na mamlaka yote aliyokuwa nayo, basi faqihi pia anaweza kuwa hivyo.(9) Faqihi Mtawala hapasi kuwa dikteta. Faqihi anayekuwa na sifa hizo huwa muadilifu. Hata hivyo uadilifu huo si ule wa kijamii, bali uadilifu ambao huporomoka kwa kusema neno moja tu la uongo au kutazama jambo la haramu. Mtu kama huyo hawezi kukiuka sheria.(10)
Mamlaka ya kiongozi na serikali
Iwapo mtu mstahiki mwenye sifa hizo mbili atasimama na kuunda serikali, atakuwa na mamlaka kama aliyokuwa nayo Mtume Mtukufu (saw) katika kuendesha masuala ya jamii na itakuwa wajibu kwa watu wote kumtii. Dhana kwamba mamlaka ya kiserikali ya Mtume (saw) yalikuwa makubwa kuliko mamlaka ya Imam Ali (as), au kwamba mamlaka ya kiutawala ya Imam Ali (as) ni makubwa zaidi ya Faqihi Mtawala, ni dhana batili na isiyokuwa sahihi. Naam, Mtume Muhammad (saw) ni mbora zaidi ya walimwengu wote, na baada yake, Imam Ali bin Abi Twalib ni mbora zaidi ya wanadamu wote. Hata hivyo wingi wa utukufu na ubora wa kiroho na kimaanawi hauzidishi mamlaka ya kiutawala. Mwenyezi Mungu ameipa serikali ya sasa mamlaka aliyokuwa nayo Mtume na Maimamu katika kizazi chake (as) katika kutayarisha majeshi, kuteuwa magavana na wakuu wa majimbo, kukusanya ushuru na kodi na kuitumia kwa maslahi ya Waislamu. Mamlaka hayo si ya mtu makshsusi, bali mtu anayekuwa kielelezo cha anwani ya "mwanazuoni muadilifu."
Tunaposema kuwa faqihi muadilifu katika kipindi cha baada ya ghaiba huwa na mamlaka kama aliyokuwa nayo Mtume (saw) na Maimamu watoharifu katika kizazi chake, watu hawapasi kudhani kwamba faqihi ana nafasi na hadhi kama ya Mtume (saw)na maimamu (sa). Kwani kadhia inayozungumziwa hapa si hadhi na daraja, bali ni suala la wajibu wa kutenda. Wilaya na mamlaka ya kuendesha mambo ya nchi na kutekeleza sheria za dini tukufu ni wadhifa mzito na muhimu na haumpi mtu nafasi na hadhi isiyokuwa ya kawaida na kumuweka katika nafasi ya mwanadamu asiye wa kawaida. Kwa maana nyingine ni kuwa mamlaka na uongozi unaojadiliwa hapa kwa maana ya serikali na kuendesha masuala ya nchi, si hadhi kama wanavyodhania watu wengi, bali ni jukumu na wajibu mzito.
Moja ya mambo yanayoshughulikiwa na Faqihi Mtawala ni kutekeleza sheria za adhabu za Kiislamu. Je, kuna tofauti katika kutekeleza sheria hizo baina ya Mtume (saw), Imam au faqihi? Je, kwa kuwa hadhi na daraja ya faqini ni chini zaidi ya nafasi ya Mtume na Imamu, anapaswa kumpiga mhalifu bakora kidogo zaidi? Hukumu ya mzinifu katika sheria za adhabu za Kiislamu ni kupigwa bakora mia moja. Je, Mtume (saw) anapotekeleza hukumu hiyo anapasa kupiga bakora 150, Imam Ali bin Abi Twalib (as) apige 100 na faqihi apige 50? Au mtawala ni mtekelezaji wa sheria za Mwenyezi Mungu sawa awe Mtume (saw), Imamu Ali Bin Abi Twalib (as), mwakilishi na kadhi aliyemteuwa yeye katika miji ya Basra na Kufa au faqihi za zama hizi?
Miongoni mwa kazi za Mtume (saw) na Amirul Muuminina Ali (as) ni kukusanya ushuru, khumsi, zaka, jizia na kodi ya ardhi za kilimo. Je, Mtume (saw) anapochukua zaka anachukua kiasi gani? Je, sehemu moja anachukua kumi na sehemu nyingine ishirini na moja? Imam Ali (as) akiwa khalifa atafanya nini? Mheshimiwa ukiwa faqihi wa zama mwenye mamlaka ya kiutendaji itakuwa vipi? Je mamlaka ya Mtume (saw) inatofautiana na ya Imam Ali (as) na faqihi katika masuala hayo?
Mwenyezi Mungu (sw) alimfanya Mtume Muhammad (saw) walii na kiongozi wa Waislamu wote, na wakati wote alikuwa na mamlaka juu ya wanadamu wote akiwemo Ali bin Abi Twalib (as). Baada ya Mtume, Imam huwa na mamlaka kwa Waislamu wote hata juu ya Imam wa baada yake. Kwa maana kwamba amri zake za kiutawala zinapaswa kutiiwa na kutekelezwa na watu wote na anaweza kuteuwa na kuuzulu viongozi wengine.
Hivyo basi, kama ambavyo Mtume Mtukufu (saw) aliamrishwa kutekeleza sheria na kanuni za Kiislamu na Mwenyezi Mungu akamfanya rais na mtawala wa Waislamu na akawajibisha kumtii, vivyo hivyo mafaqihi waadilifu wanapasa kuwa viongozi na watawala. Wanapaswa kutekeleza sheria na kusimamisha mfumo wa kijamii wa Uislamu.(11)
Serikali ni katika sheria za kwanza zinazotangulizwa mbele ya sheria nyingine
Iwapo mamlaka ya serikali yatakuwa katika fremu ya sheria tanzu za Mwenyezi Mungu itabidi serikali ya Kiislamu na utawala mutlaki aliopewa Nabii wa Uislamu (saw) vitambuliwe kuwa ni jambo lisilokuwa na maana.
Serikali ambayo ni tawi la utawala mutlaki wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) ni miongoni mwa sheria za kwanza za Uislamu zinazotangulizwa na kupewa kipaumbele zaidi ya sheria tanzu hata swala, funga na hija. Mtawala anaweza kuvunja msikiti au nyumba iliyoko katika sehemu ya kupitisha barabara na kisha kutoa fedha za fidia kwa mwenye nyumba. Vilevile anaweza kufunga misikiti inapolazimu na kubomoa msikiti wenye madhara iwapo madhara hayo hayawezi kuondolewa bila ya msikiti kuvunjwa. Serikali vilevile inaweza kuvunja kwa upande mmoja mikataba ya kisheria iliyowekeana na wananchi iwapo mikataba hiyo inapingana na maslahi ya nchi na Uislamu na inaweza kuzuia jambo lolote, sawa liwe la kiibada ama lisilokuwa la kiibada, ambalo kujiri kwake kunapingana na maslahi ya Uislamu. Aidha serikali inaweza kuzuia kwa muda utekelezaji wa ibada ya hija ambayo ni miongoni mwa faradhi muhimu za Mwenyezi Mungu, iwapo utekelezaji wake utatambuliwa kuwa ni kinyume na maslahi ya dola la Kiislamu.(12)
Utawala wa Faqihi na haki ya kudhibiti umiliki
Mali katika Uislamu ni jambo la halali na lenye mipaka maalumu na ni miongoni mwa mambo yanayosimamiwa na Faqihi Mtawala. Inasikitisha kwamba wasomi wetu hawafahamu maana ya utawala wa faqihi. Miongoni mwa mamlaka ya Faqihi Mtawala ni kuweka mipaka ya masuala hayo.
Japokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu amehalalishi umiliki wa mali lakini wakati huo huo Faqihi Mtawala anaweza kuwekea mipaka ya kiwango fulani umilikaji halali wa mali hiyo anapoona kuwa ni kinyume cha maslahi ya Waislamu na Uislamu na kuitaifisha.(13)
1- Bihar al Anwar, juz-25, Uk-116. Nahjul Balagha, hotuba ya 172. al Ihtijaj, juz-1, Uk-229.
2- Mustadrakul Wasaail, juz-17, uk-321, kitabu cha ukadhi, mlango wa sifa za kadhi, hadithi ya 33.
3- Suratul Baqarah-124
4- Wilayatul Faqih, uku 58-61.
5- Sahifeye Nur, juz-21, uk-129, tarehe 9/2/68 (29/Aprili/1989).
6- Sahifeye Nur, juz 10, uk 169-169, tarehe 17/8/58
7- Sahifeye Nur, juz 3, uk 84, tarehe 18/8/57
8- Anaashiria aya za 44-46 za suratul Haqqah zinazosema: Na kama Mtume angetuzulia baadhi ya maneno. Bila shaka tungemshika kwa mkono wa kuume. Kisha kwa hakika tungekata mshipa wake mkubwa wa moyo (tukamtoa roho).
9- Sahifeye Nur, juz 10, uk 29, tarehe 30/8/58
10- Sahifeye Nur, juz 11, uk 133, tarehe 7/10/58
11- Wilayatul Faqih, uk 92-93
12- Sahifeye Nur, juz 20, uk 170, tarehe 16/10/66
13- Sahifeye Nur, juz 10, uk 138, tarehe 14/8/58

700 /