Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu kwa mnasaba wa kuanza mwaka mpya wa 1394 Hijria Shamsia

Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehma, Mwenye kurehemu.

Ewe unayebadilisha nyoyo na macho ya watu. Ewe Mola unayefanya tadbiri ya usiku na mchana. Ewe Mola unayebadilisha mwaka na hali za watu, badili hali zetu na kuzifanya bora zaidi.”

Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu ya Fatima na baba yake na mumewe na wanawe.

Kuanza kwa mwaka mpya kumesadifiana na siku za kumbukumbu ya kufa shahidi Bibi Fatimatu Zahra (as). Mapenzi ya taifa letu kwa Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (saw) yanaandamana na mambo ya lazima kuyafanya, na nina yakini kwamba, wananchi watayachunga na kuyatekeleza. Ni matarajio kwamba mwaka mpya utaandamana na baraka za Bibi Fatima, na jina na kumbukumbu ya mtukufu huyo vitaacha taathira kubwa na ya kudumu katika maisha ya wananchi wa taifa letu katika mwaka huu mpya wa 1394. Ninatarajia kwamba kuanza kwa msimu huu wa machipuo ambako ni kuanza kwa mwaka mpya wa Hijria Shamsia kutakuwa na baraka kwa taifa la Iran na mataifa yote yanayoadhimisha sikukuu ya Nowruz.

Ninatoa salamu zangu kwa Imam wa Zama, Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake, na natumia fursa hii kumkumbuka Imam Khomeini na mashahidi na natarajia kwamba Mwenyezi Mungu atatupa baraka za maombi na dua za roho safi za wapenzi hawa.

tunatupia jicho kwa ujumla mwaka wa 1393, na tunatazama kwa ujumla mwaka huu unaoanza sasa hivi.

 Katika upande wa masuala ya ndani na wa kimataifa mwaka 1393 ulikuwa mwaka uliojaa mambo mengi kwa nchi yetu. Tumekuwa na maendeleo na pia changamoto nyingi katika mwaka huo. Ni kwa kutilia maanani changamoto hizo ndiyo maana mwanzoni mwa mwaka 1393 tuliupa jina la Azma ya Kitaifa na Uendeshaji wa Kijihadi.

Tunapotazama yaliyojiri katika mwaka 1393 tunaona kwamba, alhamdulilla, kumekuwapo azma ya kitafa. Taifa letu limeonesha azma yake kubwa katika kustahamili baadhi ya matatizo yaliyokuwepo na pia katika siku ya tarehe 22 Bahman (11 Februari wakati wa maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu), katika Siku ya Kimataifa ya Quds na katika maandamano makubwa ya siku ya Arubaini ya (Imam Hussein as), taifa leo limeonesha azma na hima yake kubwa. Uendeshaji wa kijihadi pia umeonekana katika baadhi ya sekta.

Katika maeneo ambako uendeshaji wa kijihadi ulionekana, kumeshuhudiwa pia maendeleo. Pamoja na hayo azma ya kitaifa na uendeshaji wa kijihadi si makhsusi kwa mwaka uliopita wa 1393 tu. Azma ya kitaifa na uendeshaji wa kijihadi vinahitajika kwa mwaka huu na kwa ajili ya miaka yote ijayo kwa taifa letu. Katika mwaka huu mpya wa 1394 tuna matarajio makubwa kwa taifa letu azizi na matarajio yote hayo yanaweza kutimia. 

Matarajio makubwa kwa ajili ya taifa letu katika mwaka huu ni kupata maendeleo ya kiuchumi, nguvu na heshima ya kieneo na kimataifa, ustawi wa kisayansi kwa maana yake halisi, uadilifu katika vyombo vya mahakama na uadilifu wa kiuchumi, na imani na masuala ya kiroho ambayo ni muhimu zaidi na nguzo ya yote yaliyotangulia. Kwa mtazamo wetu, matakwa na matarajio haya yanaweza kupatikana. Yote haya ni mambo yanayowezekana kwa taifa la Iran na hayako nje ya uwezo wa siasa na sera za mfumo wa Kiislamu hapa nchini. Tunao uwezo mkubwa. Kuna mengi ya kusemwa katika uwanja huu na inshaallah, nitaashiria muhimu zaidi kati ya hayo katika hotuba ya alasiri (Jumamosi).

Kitu ninachopenda kulieleza taifa letu azizi kwa wakati huu ni kwamba hayo mambo muhimu na adhimu yanaweza kupatikana lakini kwa masharti. Moja kati ya masharti hayo ni ushirikiano mkubwa na wa karibu kati ya wananchi na serikali. Iwapo ushirikiano huo mkubwa utakuwepo kutoka pande zote mbili, basi hapana shaka kuwa matarajio yetu yote yatapatikana na wananchi wataona athari zake.

Serikali ni mtumishi wa wananchi, na taifa ni mwajiri wa serikali. Kadiri kutakavyokuwapo uhusiano na ushirikiano wa karibu kati ya wananchi na serikali basi kazi zitafanyika vyema zaidi. Inabidi kuwepo hali ya kuaminiana; serikali inapaswa kulikubali taifa kwa maana yake halisi na kujua thamani, umuhimu na uwezo wake, na taifa linapaswa kuwa na imani ipasavyo na serikali ambayo ndiye mhudumu wa kazi zake.

Ninayo mengi ya kusema katika uwanja huu, na nina maagizo ambayo Mwenyezi Mungu akipenda, nitayaashiria katika hotuba yangu. Hivyo basi, katika mtazamo wangu, mwaka huu unapaswa kuitwa mwaka wa ushirikiano mpana kati ya serikali na wananchi. Ninachagua kaulimbiu hii kwa ajili ya mwaka huu: Serikali na Wananchi, Mshikamano na Maelewano. Ninatarajia kwamba kaulimbiu hii itatekelezwa kivitendo na pande zote mbili, - yaani serikali na taifa azizi na kubwa la Iran, taifa lenye hima kubwa na shujaa, taifa linaloona mbali na lenye maarifa na serikali inayohudumia wananchi, - zitaweza kutekeleza kivitendo na ipasavyo kaulimbiu hii na kuona athari na matokeo yake.

Ninaamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu aliwezeshe taifa hili kupata maendeleo katika kazi zake kubwa.

Vilevile namuomba Mwenyezi Mungu atupe taufiki ya kuhudumia taifa hili.

Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.