Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Hotuba ya Kiongozi Muadhamu katika hadhara ya makamanda na wafanyakazi wa jeshi la Jamhuri ya Kiislamu

Kwa mnasaba wa Siku ya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu (1)

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehma, Mwenye kurehemu.

Nakukaribisheni nyinyi nyote ndugu zangu wapenzi, wote mliohudhuria hapa hususan familia za mashahidi azizi, na nina matarajio kwamba inshaallah mafanikio makubwa na yenye thamani ya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi chote cha miaka mingi daima yatakuwa taji la fahari juu ya vichwa vya majmui hii yenye imani, subira na inayofanya bidii kubwa. Vilevile ninakupongezeni kwa mnasaba wa Siku ya Jeshi, nalipa mkono wa baraka Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na familia zenu na nakushukuruni kwa kuhudhuria hapa hii leo. Vilevile nakushukuruni kwa wimbo huu mzuri ambao mashairi na uimbaji wake vimevutia sana.

Hapana shaka yoyote kwamba, moja kati ya hatua na ubunifu mkubwa na wenye faida kubwa zaidi wa Imam Khomeini ni kutangaza Siku ya Jeshi.(2) Iwapo tutatazama katika siku hiyo hapa nchini, katika pembe zote za nchi, malengo yaliyokuwa katika fikra za maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu, tutaelewa kwamba hatua ya kutangazwa siku hiyo kuwa ni Siku ya Jeshi ilikuwa kazi kubwa. Ilikuwa hatua yenye faida kubwa, ya dharura na kazi ya lazima. Baadhi yenu nyinyi vijana hamkumbuki siku hizo na baadhi yenu mlikuwa bado hamjazaliwa. Kulikuwapo sababu muhimu na hatari kubwa, hata ndani ya jeshi kwa ajili ya kuliangamiza jeshi la Iran. Walikuwa wakifanya njama na kwa ajili ya kazi hiyo walikuwa wakieleza mantiki na falsafa zao. Ndani ya jeshi kwenyewe walikuwepo watu ambao kwa kutumia anwani na majina ya jeshi la kiitikadi na kitauhidi, walitaka kuliangamiza na kuliua kabisa jeshi; kulikuwepo malengo kama haya. Imam (Khomeini) alisimama kidete kukabiliana na malengo haya. Imam aliainisha kwamba jeshi linapaswa kuendelea kuwepo kwa nguvu na uwezo mkubwa zaidi na kuwa na mchango mkubwa, na mambo yote ambayo katika kipindi cha utawala wa kitaghuti yaliweza kulitenganisha jeshi na wananchi, yanapaswa kufutiliwa mbali. Jeshi kama majmui ya kimapinduzi, - na si la kimapinduzi katika maneno na madai tu, bali majmui ya kimapinduzi katika matendo, - linapaswa kuendelea kuwepo, na liendelee kuwepo katikati ya medani na kutoa mchango wake.

Kabla ya kuanza vita vya kujitetea kutakatifu ambavyo tulilazimishwa na kutwishwa, kulikuwepo matukio kadhaa, lakini katika kipindi cha vita hivyo vya miaka 8 ndipo ukweli wa mambo ulipodhihirika wazi. Katika nyanja mbalimbali- ambazo niliziashiria katika kikao hiki na katika vikao vingine, na kumbukumbu za siku hizo na yale yaliyotukia katika medani mbalimbali za vita, hususan mwanzoni mwa vita hapo mwaka 1359 (Hijria Shamsia), niliyoshuhudia kwa karibu na baadaye wakati nilipokuwa Rais wa Jamhuri ambapo sikuwa nikienda tena katikati ya medani za vita, na vilevile katika ripoti na vikao vya maamuzi- nilishuhudia yale yaliyokuwa yakifanywa na jeshi. Siku hii inapaswa kuenziwa na kumbukumbu hizi zinastahiki kulindwa na kuhifadhiwa na maana ya tarehe 29 Farvardin inapaswa kueleweka vyema. Tarehe 29 Farvardin ina maana kwamba jeshi hili ni mali ya Iran, mapinduzi na wananchi na limesimama kidete kuhudumia malengo ya wananchi na malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu. Sawasawa kabisa vijana hawa walivyoimba, jeshi limesimama wima kwa kutumia miguu ya Mapinduzi ya Kiislamu. Hii ndiyo maana ya tarehe 29 Farvardin. Kazi kubwa kama hizi zimekuwepo na zimekuwa na athari za kubakia siku zote na baada ya sasa pia zitakuwa na athari nyingi zaidi, na Mwenyezi Mungu akipenda nyinyi vijana mlioko katika anga na mazingira haya mtakuwa na kustawi mkiwa na mwelekeo huu, na inshaallah mtailetea fahari nchi yenu.

Miongoni mwa sifa za jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuwa na muono wa kimapinduzi na kidini, kuheshimu dini na kushikamana na dini. Hili ni jambo kubwa. Maana ya kushikamana na dini ni kwamba jeshi linashikamana na kuheshimu sheria na kanuni zote zilizowekwa na Uislamu kwa ajili ya vikosi vya jeshi na kwa ajili ya shughuli za jeshi. Majeshi ya dunia pale yanapojihisi kupata ushindi katika medani za vita huingia kwenye medani bila ya mipaka na kidhibiti chochote na kufanya mambo ambayo yanatia aibu. Mfano wa mambo kama hayo tumeuona katika maeneo mbalimbali. Haya hutendeka wakati majeshi hayo yanapohisi kupata ushindi na wakati huo huwa hayamuonei huruma mkubwa wana mdogo, na wakati yanapohisi hatari hufanya mambo ya aina nyingine na kuchukua hatua ambazo ni haramu katika mtazamo wa sheria tukufu za Uislamu na ni marufuku katika mtazamo wa sheria za kimataifa za dunia ya sasa. Madola makubwa yenye nguvu hayaheshimu sheria za kimataifa wala kujali kanuni za kibinadamu. Hutumia silaha zilizopigwa marufuku na kelenga raia; jinai kama hizi zinaonekana kwa wingi katika vita vyote ambako Marekani hushiriki kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja. Hii ndiyo hali ya majeshi ya dunia ya sasa. Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu na vikosi vya polisi vya Jamhuri ya Kiislamu vinaheshimu na kushikamana na sheria za Uislamu. Halichupi mipaka wakati linapopata ushindi wala halitumii nyenzo na mbinu zilizopigwa marufuku wakati wa hatari. Kwa muda mrefu miji yetu - sawa ya maeneo ya mpakani au miji mingine kama Tehran, Isfahan na kadhalika - ilikuwa chini ya mashambulizi ya kinyama ya makombora ya Saddam. Makombora hayo ya Saddam yalikuwa yakipiga vitongoji mbalimbali vya mji huu wa Tehran. Makombora hayo ambayo yalitayarishwa na nchi za Ulaya na kuuzwa yalikuwa yakiongozwa na Wamarekani na kuelekezwa kwenye shabaha. Malengo ya kijeshi yaliyopigwa picha kutoka angani yalionyeshwa kwa adui. Makombora hayo yalikuwa yakitumwa na kupiga miji yetu, yakiwakata vipandevipande raia wasio na ulinzi na kuharibu nyumba. Baada ya muda tulipata uwezo wa kulipiza kisasi na kukabiliana na adui kama anavyofanya yeye. Tulipata makombora na tungeweza kufanya kama alivyokuwa akifanya yeye (kushambulia raia na nyumba zao). Tungeweza kupiga miji iliyokuwa katika umbali wa masafa ya makombora yetu ukiwemo mji wa Baghdad. Imam (Khomeini) alitwambia, iwapo mtataka kupiga eneo lisilo la kijeshi na lisilokuwa kambi ya jeshi na kadhalika, mnalazimika kutangaza habari hiyo kwanza kupitia redio kwamba, tunataka kushambulia eneo fulani, ili raia waondoke mahala hapo. Hebu tazameni, utapata wapi duniani jeshi linaloshikamana na kanuni kama hili?

Majeshi ya nchi nyingi -au kwa mujibu tunavyojua sisi, karibu nchi zote- hayashikamani hivi na sheria. Mfano wa wazi hii leo unaoneka huko Yemen. Mumeona mfano huo wa kutoheshimu kanuni za vita huko Gaza, Lebanon na maeneo mengine. Hawafungamani na mambo kama haya lakini jeshi linaloheshimu sheria za Kiislamu linaheshimu mambo hayo. Ni kwa sababu hii ndiyo maana tumesema kwamba, hatutatumia silaha za nyuklia, kwa sababu ya kushikamana huku na kufungamana na sheria na kanuni za Kiislamu. Hii ni miongoni mwa sifa aali za jeshi la Jamhuri ya Kiislamu.

Hii leo maadui zetu wanaituhumu Jamhuri ya Kiislamu kuwa inaingilia mambo ya ndani ya huku na kule, jambo ambalo ni kinyume na ukweli. Hakuna kitu kama hicho (wanachodai). Sisi hatuingilii masuala ya nchi nyingine. Hata hivyo tutajilinda na kujihami iwapo tutashambuliwa. Tutajilinda kwa nguvu zote lakini hatuingilii mambo ya ndani ya nchi nyingine. Tunawachukia mno wale wanaowashambulia watu wasio na ulinzi, wanaoshambulia raia, wanaoangamiza watoto, wanaoua wanawake na kuharibu nyumba (za watu). Tunajitenga na watu wa aina hii na kutangaza kuchukizwa kwetu (na watu hawa). Watu hawa hawaujui kabisa Uislamu na hawana ubinadamu. Sifa ya jeshi letu ni kwamba linashikamana na misingi ya Uislamu na sheria za Mwenyezi Mungu zilizowekwa katika kila kitu hata katika vita na wakati wa amani. Hii ni miongoni mwa sifa za jeshi letu. Hii ndiyo sababu ya kupendwa vikosi vya jeshi na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi (SEPAH) baina ya wananchi. Wananchi wanaliona jeshi likifikiria kama wao na kutenda kama wanavyotenda wao, lina imani na itikadi zinazofanana na zao na linaumizwa na mambo yanayowaumiza wananchi; suala hili linazidisha uhusiano baina ya wananchi na vikosi vya jeshi. Hii ni miongoni mwa sifa za jeshi letu.

Sifa nyingine inayopaswa kutiliwa maanani na vikosi vya majeshi yetu na kwa bahati nzuri inapewa mazingatio kama inavyoshuhudiwa kikamilifu, ni utekelezaji wa aya tukufu ya Qur’ani inayosema:

وَ اَعِدّوا لَهُم مَا استَطَعتُم مِن قُوَّةٍ وَ مِن رِباطِ الخَیلِ تُرهِبونَ بِه‌ عَدُوَّ اللهِ وَ عَدُوَّکُم

Na waandalieni nguvu kadiri mtakavyoweza na kwa farasi waliofungwa, ili mumtishe adui wa Mwenyezi Mungu na adui yenu”.(3) Maana ya aya hii ni kwamba msighafilike, maana yake ni kuwa iwapo mtashambuliwa na adui msipate hasara kutokana na uhaba wa zana, uchache wa silaha na kutokuwa tayari; kwa sababu hasara yenu ni hasara ya taifa na hasara ya Uislamu. Kwa msingi huo nimesema maendeleo liliyoyapata jeshi letu hadi sasa katika uwanja huu ni kigezo kizuri. Kwa maana kwamba katika upeo wa taifa, licha ya kuwa nchi yetu iko katika kiwango kinachokubalika na kikubwa duniani katika upande wa maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia, lakini katika majmui ya maendeleo yaliyopatikana hapa nchini, maendeleo ya utengenezaji wa silaha yanahesabiwa kuwa miongoni mwa mafanikio makubwa zaidi. Kiasi tulichoweza kusonga mbele katika utengenezaji wa silaha na zana hapa nchini katika miaka hii, katika kipindi hiki, na katika muda huu mfupi, chini ya mashinikizo na wakati wa vikwazo na uhaba wa vyanzo, ni kazi adhimu na kazi kubwa sana.

Kwa bahati nzuri, jeshi katika sekta mbalimbali ama kwa njia ya moja kwa moja au kwa kutumia taasisi za kielimu na teknolojia, limeweza kufanya kazi kubwa na kazi hiyo inabidi idumishwe na kuendelezwa. Ninachokitilia mkazo hapa ni kuwa, maendeleo ya nchi katika nyanja za kutengeneza silaha na nyanja za utayarifu wa kivita yanapaswa kudumishwa. Adui yetu hataki kuona jambo hili. Hii leo moja kati ya nyenzo zinazotumiwa kuishinikiza Jamhuri ya Kiislamu ni suala la makombora, suala la ndege zisizo na rubani, suala la zana na uwezo wa kijeshi na mambo mengine ambayo tumeyapata hapa nchini kutokana na ubunifu wa vijana wetu bila ya kuomba msaada kutoka kwa huyu au yule. Hawataki kuona maendeleo haya, wanataka kusitisha jambo hili. Mantiki sahihi na ya akili na busara inayoungwa mkono na aya ya Qur’ani inatwambia kwamba, njia hii inabidi iendelezwe.

Upande unaokabiliana nasi, kwa ufidhuli kamili, unatishia kutushambulia kijeshi, kwa ufidhuli unatoa vitisho vya kutushambulia. Kwa muda fulani walikuwa kimya, lakini siku chache zilizopita mmoja wao alifungua mdomo na kuzungumzia machaguo yaliyoko mezani na chaguo la kijeshi. Tazama, wanavyojigamba, wanafanya makosa mengi kama haya kisha wanasema Jamhuri ya Kiislamu lazima inyang’anywe uwezo wa kujilinda. Je maneno haya wanayosema si ya kipumbavu? Hata kama wasingetoa vitisho vya waziwazi kama hivi dhidi yetu basi tuliwajibika kutafakari kwa mujibu wa aya ya:

 وَاَعِدُّوا لَهُم مَا استَطَعتُم مِن قُوَّةٍ و مِن رِباطِ الخَیل (4). Hata kama wasingetoa vitisho basi tulipaswa kuwa macho na kuzidisha utayarifu wetu seuze hivi sasa wanatoa vitisho waziwazi. Katika upande mmoja wanatoa vitisho na katika upande mwingine wanasema nyinyi hampaswi kutengeneza makombora, hampaswi kufanya hili na hampasi kufanya lile. Daima wanatoa amri zisizo na mashiko na za kipumbavu katika anga ya propaganda au katika maamuzi ya kimataifa. Hapana, kwanza Jamhuri ya Kiislamu imethibitisha na kuonesha kuwa, ina uwezo kamili wa kujilinda na inatekeleza mambo yake kwa nguvu na uwezo mkubwa. Taifa letu lote litashikamana mithili ya ngumi imara na kupambana mbele ya mchokozi, mbele ya mvamizi na dhidi ya mhujumu asiye na mantiki. Katika suala la kujilinda, taifa letu lina mshikamano kamili na hakuna kitu kinachoweza kuathiri mshikamano huo. Hiyo ni mosi. Pili ni kwamba Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuwa tayari na italinda utayarifu wake.

Asasi zote za Jamhuri ya Kiislamu - kuanzia Wizara ya Ulinzi hadi taasisi za jeshi, Sepah na asasi nyingine – zinapaswa kulitambua jambo hili kuwa ni amri na desturi. Utayarifu wetu unapaswa kuongezeka siku baada ya siku katika nyanja za silaha, katika nyanja za uratibu na mipango na katika uwanja wa kile chenye taathira kubwa zaidi katika vikosi vya jeshi, yaani utayarifu wa kiroho. Kwa bahati nzuri hapa nchini vikosi vyetu, vijana wetu na mashujaa wetu hawana upungufu wowote katika uwanja huu, hawana upungufu na kwa bahati nzuri hatujihisi kuwa na uhaba na upungufu katika upande wa kiroho. Malengo ya mapinduzi, malengo ya tarehe 29 Farvardin, malengo ya kuasisiwa jeshi la Sepah yaliyobuniwa na Imam (Khomeini), yote yametimia. Moyo, ujasiri na utayarifu mkubwa! Kwa sasa vijana wengi ambao hawakuona Mapinduzi ya Kiislamu, hawakumuona Imam (Khomeini), hawakuwepo katika siku za vita wala hawana kumbukumbu za siku hizo, hawa vijana wa leo ndani ya jeshi wananitumia ujumbe kupitia njia mbalimbali kwamba wako tayari kujitolea. Rubani wa jeshi la Jamhuri ya Kiislamu anatuma ujumbe, rubani wa kikosi cha anga anatuma ujumbe kwa njia nyingine, afisa wa jeshi la majini au la nchi kavu anatuma ujumbe; wote wanatangaza utayarifu wao. Kila jeshi linalokuwa na moyo na ujasiri mkubwa, kila kikosi kinachokuwa na moyo kama huu hapana shaka kitasonga mbele katika makabiliano na katika mitihani na misukosuko. Mnapaswa kusonga mbele na moyo na ujasiri huu. Kwa msingi huo, kulinda uoni wa mbali, kulinda mwelekeo sahihi, utayarifu unaohitajika, kuwa na moyo na ujasiri na kuzidisha zana na silaha na kuwa tayari kwa ajili ya vita ni miongoni mwa mambo muhimu ambayo vikosi vya jeshi vinapaswa kuwa nayo.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran si tishio kwa nchi yoyote. Hatujawahi kuwa tishio kwa majirani zetu seuze kwa (nchi) za maeneo ya mbali. Ukweli huu unaoneshwa waziwazi na historia yetu ya sasa. Hata wakati baadhi ya majirani zetu walipoamiliana nasi kwa mwenendo usiostahiki kufanywa na jirani, tulijizuia na kuwa na subira. Jamhuri ya Kiislamu haishambulii wala haitashambulia nchi yoyote.

Kwa sasa Wamarekani, na nyuma yao watu wa Ulaya na baadhi ya vibaraka wao wamebuni ngano ya suala la nyuklia na silaha za nyuklia (dhidi ya Iran) ili waweze kusema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ni tishio (kwa nchi nyingine). La hasha, tishio ni Marekani yenyewe. Hii leo tishio kubwa zaidi duniani ni Marekani ambayo, bila ya kidhibiti na bila ya kuheshimu na kufungamana na kanuni za kibinadamu na sheia za dini, inaingilia mambo ya nchi nyingine mahala popote inapoamua kufanya hivyo. Inaingilia mambo ya eneo hilo na kuvunja amani. Marekani imeifanya dunia kuwa mahala pasipo na amani. Katika eneo letu hili (Mashariki ya Kati) mvunjaji wa amani ni utawala wa Kizayuni wa Israel ambao ni mbwa aliyeko kwenye myororo wa Marekani. Hawa ndio wanaovunja amani duniani. Jamhuri ya Kiislamu haivunji amani ya dunia wala haivunji amani ya eneo la Mashariki ya Kati. Si hayo tu bali hata haivunji amani ya majirani zake. Wakati mwingi pia inastahamili mienendo mibaya ya baadhi ya majirani zake. Uvunjaji wa amani unafanywa na madola yasiyodhibitiwa ambayo yanadhibiti kila mahala. Hivi sasa matukio haya yanayomliza na kumtoa machozi mwanadamu yanajiri huko Yemen na Wamarekani wanamuunga mkono dhalimu, Wamagharibi pia wanamuunga mkono dhalimu. Hawa ndio wavunjaji wa amani. Hawa ndio wanaovuruga amani na usalama wa nchi mbalimbali na ndio wanaovunja amani ya mazingira ya maisha ya mwanadamu. Uvunjaji wa amani unafanywa na watu hawa. Jamhuri ya Kiislamu - kwa ajili yake yenyewe na kwa ajili ya nchi nyingine – inaitambua amani na usalama kuwa ni neema kubwa ya Mwenyezi Mungu na inasimama kidete kulinda na kutetea usalama na amani yake. Wito huu daima unapaswa kuwa katika masikio ya maafisa wa vikosi vya jeshi. Kulinda usalama na amani, kulinda usalama mipakani na kulinda usalama wa wananchi ni majukumu ya maafisa wanaofanya kazi katika uwanja huu.

Namuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu avipe taufiki zaidi vikosi vya jeshi la Iran na awape taufiki nyinyi vijana ili muweze kutekeleza majukumu yenu na mchango. Majukumu hayo si kupigana vita pekee, bali pia kuwa tayari, kuleta maendeleo, kuijenga nafsi, kuwa na mchango katika kuboresha asasi mbalimbali na kadhalika; haya ni katika mambo makubwa. Hata hivyo iwapo kutatokea mapigano basi kushiriki katika medani za vita ni katika utayarifu na sehemu ya mitihani na kadhalika. Ninatarajia kwamba inshaallah, Mwenyezi Mungu atakupeni taufiki katika mambo yote.

Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh

1) Kabla ya kuanza hotuba ya Kiongozi Muadhamu, Meja Jenerali Sayyid Ataullah Salehi, Kamanda Mkuu wa Majeshi ya Iran alitoa ripoti.

2) Rejea kwenye Sahifeye Emam, juzuu ya 7 ukurasa wa 20, ujumbe kwa taifa la Iran na kutangazwa Siku ya Jeshi (26/1/1358).

3) Sura ya al Anfal, sehemu ya aya ya 60.

4) Aya ya 60 ya Suratul al Anfal.