Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Hotuba za Swala ya Idul Fitr, 1 Shawwal 1436 Muswalla wa Imam Khomeini Tehran (2015/07/18)

Bismillahir Rahmanir Rahiim
Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe vyote. Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliyeumba mbingu na ardhi, na akafanya giza na mwangaza. Tena baada ya haya waliokufuru wanawafanya wengine sawa na Mola wao. Tunamhimidi, kumsabihi na kutubu kwake na tunamswalia na kumtumia salamu mpendwa, mwenye uzao bora na mbora wa viumbe wake, Bwana  na Mtume wetu Abul Qasim al-Mustafa, Muhammad na (tunaswali na kuwatumia salamu pia) Aali zake wema, watoharifu na wateule, viongozi walioongozwa na maasumiina (wasiotenda dhambi) na hasa yule ambaye amehifadhiwa na Allah ardhini (duniani).
Ninakupongezeni nyinyi ndugu na dada, taifa pendwa la Iran na Waislamu wote kote ulimwenguni kwa mnasaba huu wa heri ya Dul Fitr. Ninakuusieni nyinyi wasimamishaji Swala na mimi mwenyewe tuzingatieni taqwa na uchamungu, kuchunga nafsi na kuepuka dhambi.
Mwezi wa Ramadhani wa mwaka huu ulikuwa mwezi wa baraka kwa maana yake  halisi. Baraka za Mwenyezi Mungu zililinyeshea taifa hili na alama zake zilionekana katika funga za siku ndefu na zenye joto kali, katika mahafali nyingi za Qur'ani zilizofanyika katika pembe zote za nchi na katika vikao vikubwa vya dua na kutawasali – ambapo maelfi ya vijana kwa wazee na wanaume kwa wanawake walinyanyua mikono ya dua na maombi na kuzungumza na Mungu wao kwa ikhlasi na unyenyekevu –, katika futari nyingi ambazo kwa bahati nzuri zimeenea sana katika miaka kadhaa iliyopita, misikitini, njiani, barabarani na hatimaye kwenye maandamano makubwa ya Siku ya  Quds. Hizi ni alama za rehema ya Mwenyezi Mungu. Wananchi waliofunga saumu ambao usiku uliotangulia walikuwa wamekesha wakihuisha usiku wa tarehe 23 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani na usiku wa Lailatul Qadr, walishiriki kwenye maandamano haya makubwa katika siku yenye joto kali ya msimu wa joto huku wakiwa wamefunga. Hizi ndizo njia sahihi za kulielewa taifa la Iran; hili ndilo taifa la Iran. Hili ndilo taifa la Iran ambalo mwezi wa Ramadhani huwa hivi katika mihirabu ya ibada  na huonekana na kujidhihirisha hivi vingine katika uwanja wa makabiliano na mapambano dhidi ya uistikbari na ubeberu. Taifa letu halipasi kufahamika kupitia ndimi za uchochezi za watu wengine. Taifa letu linapasa kufahamika kupitia kwake lenyewe, nara zake, harakati zake na kupitia madhihirisho haya adhimu. Hili ndilo taifa la Iran. Kile ambacho maadui wanajaribu kukidhihirisha kuwa ndilo taifa la Iran kupitia propaganda, na kwa bahati mbaya kinakaririwa na baadhi ya watu walio na ufahamu mbaya, ni upotovu na makosa. Taifa la Iran ni lilelile taifa mbalo lilionyesha pande na viungo vyake tofauti katika mwezi huu wa Ramadhani. Inshaallah leo nyote mtapata shahada ya kufuzu. Leo Inshaallah kwa mnasaba wa Idi, taifa la Iran litapewa shahada ya kufuzu (kufaulu) ibada hii kutoka kwenye chanzo (chimbuko) la neema na rehema ya Mwenyezi Mungu. Inshaallah baadhi yenu mbali na kupokea shahada ya kufaulu, mtapewa pia zawadi, kupandishwa cheo na kuimarika kimaanawi na kiroho. Nara na kaulimbiu za taifa la Iran zimeonyesha mielekeo. Katika Siku ya Quds, nara za 'mauti kwa Israel' na ' mauti kwa Marekani' ziliitikisa nchi, na hazikuhusu Tehran na miji mikubwa tu bali nchi nzima ilikuwa chini ya mwavuli wa harakati hii adhimu.
Ewe Mwenyezi Mungu! Kwa rehema na neema yako litakabalie taifa la Iran. Ewe Mwenyezi Mungu! Literemshie taifa hili taufiki, rehema na neema zako. Ewe Mwenyezi Mungu! Warehemu na kuwaghufiria mashihidi wetu wapendwa, Imam mpendwa na wale wote waliolisaidia taifa katika njia hii.
Bismillahir Rahmanir Rahiim
Naapa kwa Zama! Hakika binaadamu bila ya shaka yumo katika hasara,
Ila wale walioamini, na wakatenda mema, na wakausiana kwa haki, na wakausiana kusubiri. (1)
Bismillahir Rahmanir Rahiim
Na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe (vyote). Na swala na salamu zimuendee Bwana na Nabii wetu Abul Qassim al-Mustafa Muhammad, na swala ziwaendee Maimamu wa Waislamu na watetezi wa wanyonge. Amirul Mu'mineen, na Bibi wa Wanawake wa ulimwengu, na al- Hassan na al-Hussein ambao ni wajukuu wa rehema na Maimamu wa wongofu, na Ali bin al-Hussein Zeinul Abideen, na Muhammad bin Ali, na Ja'far bin Muhammad na Musa bin Ja'ffar na Ali bin Musa na Muhammad bin Ali na Ali bin Muhammad na al-Hassan bin Ali na mrithi, mwongozaji aliyeongozwa sawasawa, (hawa Maimamu) ni hoja Zako kwa waja Wako na walinda amana Wako kwenye ardhi (miji) Zako.
Salamu na pongezi kwa ndugu na dada wasimamishaji swala sambamba na kuwausieni taqwa, ni matamshi yetu ya kwanza katika hotuba ya pili.
Matukio ya eneo letu katika mwezi huu wa Ramadhani na kabla ya hapo, yalikuwa na yangali ni matukio machungu. Inasikitisha kwamba mikono miovu imeufanya mwezi wa Ramadhani kuwa mchungu mno kwa watu wengi wa eneo la Mashariki ya Kati. Huko Yemen, Bahrain, Palestina, Syria Waislamu wengi waumini walipitia siku ngumu na kuwa na funga ngumu kutokana na maovu yaliyotendwa na maadui. Mambo haya yote ni muhimu kwa taifa letu.
Suala jingine pia ni suala letu la ndani ambalo ni suala la mazungumzo ya nyuklia. Nitazungumzia nukta kadhaa kuhusiana na suala hili. Nukta ya kwanza ni kuwashukuru wahusika wote wa mazungumzo haya marefu na magumu, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri na hasa timu ya Iran katika mazungumzo hayo ambayo kwa hakika ilifanya jitihada na juhudi kubwa. Sawa matini iliyotayarishwa (kwenye mazungumzo), ipasiswe katika mkondo wake wa kisheria ulioainishwa au la, watapata malipo yao kwa Mwenyezi Mungu. Niliwaambia jambo hilihili pia ndugu hawa (nilipokutana nao) kwa karibu. Bila shaka ili kupasishwa matini hiyo, kuna hatua za kisheria zilizoainishwa ambazo zinapaswa kupitiwa na zitapitiwa, Inshallah. Matarajio yetu ni kuwa wahusika, watazingatia maslahi – maslahi ya nchi, maslahi ya taifa – na hivyo kuweza kuwasilisha pia kwa fahari mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kile watakachokuwa wamekiwasilisha mbele ya taifa.
Nukta nyingine ni kuwa matini hii iwe itapitishwa au la, kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu, haitaruhusiwa kutumiwa vibaya kwa namna yoyote ile. Hakuna mtu atakayeruhusiwa kudhuru misingi mikuu ya Mfumo wa Kiislamu. Uwezo wa ulinzi na maeneo ya usalama (kijeshi) yatalindwa kwa neema zake Mwenyezi Mungu, japo tunajua vyema kwamba maadui wanategemea sana nukta hii mahsusi. Jamhuri ya Kiislamu katika uwanja wa kulinda uwezo wake wa kiulinzi na kiusalama – tena katika mazingira haya ya vitisho ambayo imesababishiwa na maadui wake – kamwe haitasalimu amri mbele ya matakwa ya ziada (yasiyo ya kimantiki) ya adui.
Nukta nyingine ni kuwa, matini iliyotayarishwa iwe itapitishwa au la, sisi hatutaacha kuwaunga mkono marafiki zetu katika eneo la Mashariki ya Kati: Hatutaacha kuyaunga mkono mataifa madhlumu ya Palestina, Yemen, Bahrain na mataifa na serikali za Syria na Iraq na wananchi madhlumu wa Bahrain na mujahidina wakweli wa Lebanon na Palestina. (Mataifa haya) daima yataendelea kupata uungaji mkono wetu.
Nukta nyingine ni kuwa kwa mazungumzo haya na matini iliyotayarishwa, kwa vyovyote vile, siasa zatu mkabala na serikali ya kiistikbari (kiburi) ya Marekani hazitabadilika hata kidogo. Kama tulivyosema mara kwa mara, sisi hatufanyi mazungumzo na Marekani kuhusiana na masuala mbalimbali ya kimataifa na kieneo. Hatufanyi mazungumzo kuhusiana na masuala ya pande mbili. Baadhi ya wakati tunafanya mazungumzo kuhusu masuala maalumu, kama (kwa mfano) suala hili la nyuklia, kwa mujibu wa maslahi; na si suala hili pekee. Kabla ya mazungumzo haya pia kulikuwepo na mazungumzo mengine ambayo niliyaashiria katika hotuba zangu nyingine za hadhara. Siasa za Marekani katika eneo zinatofautiana na za Jamhuri ya Kiislamu kwa digrii (nyuzi) 180 (mia kwa mia). Wamarekani wanaituhumu Hizbullah na Mapambano ya Lebanon – ambalo ni jeshi la ulinzi wa kitaifa linalojitolea zaidi katika nchi – kuwa ni magaidi. Je, kuna dhulma kubwa zaidi kuliko hii? Wakati huohuo katika upande wa pili, wanaiunga mkono serikali ya kigaidi ya Kizayuni inayoua watoto wadogo. Tunawezaje kuamiliana na siasa kama hizi, tunawezaje kufanya mazungumzo na tunawezaje kufikia mapatano? Kuna mifano mingine pia ambayo nitaizungumzia sehemu nyingine.
Nukta nyingine ni kuhusiana na majitapo ya Marekani katika siku kadhaa zilizopita. Katika siku kadhaa zilizopita baada ya kumalizika mazungumzo, hawa mabwana viongozi wa Marekani – wanaume kwa wanawake – wamekuwa wakijitapa, na kila mmoja wao akijitapa kwa lugha tofauti. Ni wazi kuwa sisi hatuna tatizo na majitapo hayo. Matatizo yao ya ndani ndiyo yamewalazimu kujitapa na (kudai) kuwa, ndio, sisi tumeivuta (tumeilazimisha ) Iran kuketi kwenye meza ya mazungumzo, tumeilazimisha Iran kusalimu amri, tumeizuia Iran kutengeneza silaha  za nyuklia, sisi tumepata fursa fulani, na mambo kama hayo! Ukweli wa mambo ni tofauti kabisa. Wanasema tumeizuia Iran kupata (kutengeneza) silaha za nyuklia. Silaha za nyuklia za Iran hazina uhusiano wowote na mazungumzo na Marekani au nchi nyingine isiyokuwa Marekani; wao wenyewe pia wanalijua vizuri suala hilo. Wakati mwingine wao huzungumzia umuhimu wa fatwa (yetu) ya kuharamisha silaha za nyuklia. Sisi, kwa msingi wa hukumu (mafundisho) ya Qur'ani na sheria za Kiislamu, tunaamini kuwa uzalishaji, urundikaji na utumiaji wa silaha za nyuklia ni haramu na wala hatuwezi kufanya mambo haya. Suala hili haliwahusu wao na wala halina uhusiano na mazungumzo haya. Hao wenyewe wanajua kwamba huu ndio ukweli – wanajua kwamba jambo linaloizuia Iran kutengeneza silaha za nyuklia sio vitisho wala maneno yao makali, bali ni kizuizi cha kisheria. Wanajua umuhimu wa Fatwa hii –, pamoja na hayo lakini bado wanasema kuwa sisi ndio (tulioizuia). Hawawaambii ukweli watu wao, hawasemi ukweli. Katika masuala mengine mbalimbali, husema sisi tumefanya hivi kuhusiana na sekta ya nyuklia (ya Iran), tulisema hivi (na) kuifanya Iran isalimu amri; lakini wataiona Iran ikisalimu amri kwenye ndoto zao tu. Marais wengine watano (wa Marekani) tokea mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi hadi leo, waliokuwa na matumaini ya kuilazimisha Jamhuri ya Kiislamu isalimu amri, ima wamekufa au wametoweka kwenye historia, (na) nyinyi pia kama walivyokuwa wao, nyinyi pia kamwe hamtaona matumaini ya kuilazimisha Iran ya Kiislamu isalimu amri, yakithibiti na kutimia.
Kulikuwa na nukta moja kwenye maneno ya Rais wa Marekani katika siku chache zilizopita, nayo ni ya kukiri makosa yaliyofanywa na nchi hiyo.  Hata hivyo, hii ni sehemu ndogo tu ya makosa (hayo). Alikiri kwamba tarehe 28 Mordad (Agosti 19, 1953) Wamerekani walifanya makosa (kwa kupanga mapinduzi dhidi ya serikali) nchini Iran. Alikiri kwamba kwa kumsaidia Saddam Hussein, Wamarekani walikosea. Aliashiria masuala mawili matatu hivi, lakini hakugusia makumi mengine ya makosa (yaliyofanywa na Wamarekani). Hakuzungumzia miaka 25 ya utawala wa kidhalimu na kidikteta wa Pahlavi wa Pili, mateso, uporaji, mauji, jinai, maafa, kupoteza heshima ya taifa la Iran na kukanyagwa kwa maslahi ya ndani na nje ya taifa la Iran kulikofanywa na Marekani. Hakusema udhibiti wa Wazayuni, hakuzungumzia kuuawa wasafiri wa ndege ya abiria iliyotunguliwa kwa kombora kutoka baharini na mambo mengine mengi lakini alikariri makosa machache tu. Mimi ninataka kuwanasihi mabwana hawa jambo moja: Leo nyinyi baada ya kupita miaka mingi ya tukio la tarehe 28 Mordad au vita vya miaka minane na kujitetea Jamhuri ya Kiislamu mnakiri kwamba mlifanya makosa. Mimi ninataka kusema kuwa hivi sasa pia bado mnafanya makosa. Hivi sasa pia mngali mnafanya makosa katika sehemu tofauti za eneo hili hasa kuhusiana na Jamhuri ya Kiislamu na taifa la Iran.  Miaka mingine michache ijayo mtu mwingine atakuja na kukiri makosa yenu haya mnayoyafanya, kama mnavyokiri nyinyi leo kuhusiana na makosa yaliyofanywa na viongozi wenu wa zamani. Nyinyi pia mnafanya makosa; amkeni, tokoni kwenye makosa, eleweni ukweli wa mambo. Wanafanya makosa makubwa katika eneo la Mashariki ya Kati. Jambo ninalotaka kuwaambia wananchi wa Iran ni kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa taufiki yake Mwenyezi Mungu na uwezo wake ni imara na yenye nguvu, na inazidi kuwa na nguvu siku baada ya nyingine. Ni miaka 10 au 12 hivi ambapo serikali (madola) sita kubwa duniani – ambazo zinahesabiwa kuwa miongoni mwa nchi zilizo na nguvu kubwa zaidi duniani kwa mtazamo wa utajiri wa uchumi na msuala mengine, zimeketi mkabala na Iran kwa lengo la eti kuilazimisha iache kufuatilia miradi yake ya nyuklia; wamelisema hili waziwazi. Lengo lao hasa ni kufungua kabisa nati na bolti za sekta ya nyuklia hapa nchini. Waliwaambia haya pia waziwazi maafisa wetu miaka iliyopita na sasa pia wangali wana matumaini hayo. Miaka 10 au 12 ya mivutano na Jamhuri ya Kiislamu, natija yake imekuwa hii kwamba madola haya sita yenye nguvu leo yamelazimika kustahamili mzunguko wa maelfu ya mashinepewa hapa nchini. Yamelazimika kustahamili kudumishwa kwa kiwanda (sekta/teknolojia) hiki nchini. Yamelazimika kustahamili kudumishwa kwa utafiti na kustawishwa kwa sekta hii. Utafiti na ustawi wa sekta ya nyuklia utaendelea, maendeleo ya sekta ya nyuklia yataendelea kuwepo. Hili ndilo jambo ambalo kwa miaka mingi walifanya juhudi (za kulizuia) (lakini) leo wameliweka kwenye karatasi na wanasaini (kuonyesha) kuwa sisi hatuna pingamizi. Hili lina maana gani nyingine ghairi ya kuonyesha nguvu za taifa la Iran? Hili linatokana na uimara wa taifa, mapambano ya wananchi na ujasiri pamoja na uvumbuzi wa wasomi wetu wapendwa. Rehema ya Mwenyezi Mungu iwe juu ya (wanasayansi mashahidi wa nyuklia kama vile) akina Shahriyari, akina Ridhainejad, akina Ahmadi Roshan na akina Ali Muhammadi. Rehema ya Mwenyezi Mungu iwe juu ya mashahidi wa nyuklia, familia zao na juu ya taifa ambalo husimama imara kutetea neno lake la haki na kusisitiza kupewa haki yake.
Ninazungumzia maudhui nyingine ambayo itakuwa nukta ya mwisho mimi kuizungumzia. Huyu bwana (Rais wa Marekani) amesema kuwa anaweza kuliangamiza jeshi la Iran. Wazee wetu wa kale (wahenga) walikuwa wakiyataja maneno kama hayo kuwa ni 'majitapo mbele ya wageni' (yaani majigambo ya wapumbavu mbele ya watu wasiowajua vizuri – wasioelewa vyema udhaifu na historia yao mbovu). (2) Mimi sitaki kusema lolote katika uwanja huu. Wale watakaosikia maneno haya, kama wanataka kufahamu vizuri, kama wanataka kunufaika vyema na uzoefu wao, wanapasa kufahamu. Sisi hatukaribishi vita vyovyote. Hatuanzishi vita vyovyote na wala hatutatangulia. Lakini kama vita vitazuka hapa, mtu atakayetoka kwenye vita hivyo hali ya kuwa ameshindwa na kudhalilika ni Marekani mchokozi na mtenda jinai.
Bismillahir Rahmanir Rahiim
Itakapokuja nusra ya Mwenyezi Mungu na ushindi. Na ukaona watu wanaingia katika dini ya Mwenyezi Mungu makundi makundi. Basi zisabihi sifa za Mola wako na umtake maghufira; hakika Yeye ni Mwingi wa kukubali toba. (3)
Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

1- Suratul Asr aya 1-3.
2- Kicheko cha watu wanaohudhuria ibada ya Swala ya Idi.
3- Suratu Nasr, aya ya 1-3.