Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ujumbe wa Nairuzi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu 1395 Hijria Shamsia

Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, ametoa ujumbe wa Nairuzi kwa taifa la Iran kwa mnasaba wa kuanza mwaka 1395 Hijria Shamsia na kuuita mwaka huu kuwa ni mwaka wa "Uchumi Ngangari, Hatua na Vitendo."
Matini kamili ya ujumbe huo ni hii ifuatayo:

سم الله الرحمن الرحیم
یا مقلّب القلوب و الابصار، یا مدبّر اللّیل و النّهار، یا محوّل الحول و الاحوال، حوّل حالنا الی احسن الحال
Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu
Ewe Mgeuzaji wa nyoyo na macho! Ewe unayeendesha usiku na mchana!
Ewe Mbadilishaji wa mwaka na hali! Badilisha hali zetu kuwa bora ya hali.
Sala na salamu za Allah zimshukie Swiddiqah al Twahirah, Fatimatu al Mardhiyyah binti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, amani ya Allah iwe juu yake na Aali zake. Amani iwe juu ya Walii Mkubwa zaidi wa Mwenyezi Mungu, roho zetu ziwe wahanga wake, na Mwenyezi Mungu aharakishe faraja yake.
Ninatoa mkono wa sikukuu ya Nairuzi kwa familia zote za Kiirani na Wairani walioko katika kila kona ya dunia. Nakutakieni sikukuu iliyojaa baraka wananchi wenzangu wapendwa. Mkono wangu wa baraka zaidi uziendee hasa familia azizi za mashahidi, majeruhi wapendwa wa vita na familia zao na watu wote wanaojitolea katika njia ya Mwenyezi Mungu. Ninaitumia fursa hii kuwakumbuka kwa wema mashahidi wetu watukufu na Imam wetu azizi.
Mwaka huu mpya ulioanza hivi punde - mwaka 95 - (Hijria Shamsia) umepata baraka za jina la Bibi Fatimatu Zahra (amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake), mwanzo na mwisho wake. Mwanzo wa mwaka huu umesadifiana na maadhimisho ya kukumbuka kuzaliwa mtukufu huyo kulingana na mwaka wa Hijria Qamaria, na mwisho wake pia itakuwa vivyo hivyo. Hivyo ni matumaini yetu kwamba kwa matakwa Yake Mwenyezi Mungu mwaka huu wa 1395 (Hijria Shamsia) utakuwa mwaka wenye baraka tele za Bibi Fatimatut Zahra kwa taifa la Iran na tutaweza kufaidika na kupata somo la kimaanawi kutoka kwa mtukufu huyo, na kustafidi vizuri na miongozo ya busara ya mtukufu huyo na maisha yake.
Mwaka ulioisha - mwaka 1394 - kama ilivyokuwa kwa miaka mingine yote, uliandamana na mambo matamu na machungu pamoja na panda shuka nyingi na hilo ni jambo la kawaida katika maisha. Mwaka huo uliandamana na matukio machungu kuanzia lile la Mina, hadi matukio matamu kama maandamano makubwa ya Bahman 22 (Februari 11, kileleni cha sherehe za Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran) na hadi kwenye uchaguzi wa tarehe 7 Isfand (Februari 26) na vilevile uzoefu wa JCPOA (makubaliano ya nyuklia baina ya Iran na kundi la 5+1) na pia kuanzia kwenye matumaini yalijitokeza hadi kwenye wasiwasi ulioambatana na jambo hilo. Yote hayo ni miongoni mwa matukio ya mwaka huo, na hiyo ndiyo hali inavyokuwa katika miaka yote.
Miaka na siku za maisha ya mwanadamu huandamana na fursa mbalimbali na pia huwa na vitisho tofauti. Vipaji vyetu vinapaswa vionekane kupitia kutumia vizuri fursa tunazopata na hata vitisho tunavyokumbana navyo, ili kuvigeuza vitisho hivyo kuwa fursa nzuri kwetu. Hivi sasa tumeingia kwenye mwaka 95. Katika mwaka huu, kama ilivyo mara zote, zitakuweko fursa mbalimbali na vitisho pia. Kila mmoja wetu anapaswa kufanya juhudi ya kuhakikisha tunatumia vizuri fursa tutakazopata mwaka huu kwa maana halisi ya neno hilo ili mwanzo wa mwaka wa nchi yetu uwe tofauti sana mwisho wa mwaka huu.
Kuna matumaini kuhusu mwaka huu wa 1395. Wakati mtu anapoangalia hali na mambo mbalimbali, anapata matumaini mazuri. Inabidi juhudi zifanyike ili kufanikisha kivitendo matumaini hayo. Inabidi kufanyike kazi usiku na mchana na kufanyike jitihada kubwa bila ya kusita na wala kukwama sehemu yoyote ile. Jambo hasa linalotakiwa ni kuwa, taifa la Iran lihakikishe linafanya mambo ambayo yatalitoa katika hali ya kuathiriwa na vitisho vya maadui na uadui wao. Tunapaswa tuhakikishe kuwa tunajiwekea kinga madhubuti ambayo itatufanya tusidhuriwe na vitisho vya maadui. Yaani tuhakikishe kuwa uwezekano wa kudhuriwa na vitisho hivyo ni wa asilimia sifuri.
Ninavyoamini mimi ni kuwa, suala la uchumi ndilo la kupewa kipaumbele cha kwanza kabisa. Yaani wakati mtu anapoangalia masuala yenye vipaumbele anaona kuwa kati ya vipaumbele vyote hivyo, suala la uchumi ndilo la haraka zaidi na la karibu zaidi. Kama kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu, wananchi na serikali na viongozi wa sekta mbalimbali watafanikiwa kufanya kazi nzuri, kwa njia sahihi na inavyotakiwa katika masuala ya kiuchumi, basi ni matumaini yetu kuwa jambo hilo litaathiri pia katika masuala mengine kama ya kijamii, kama vile matatizo ya kijamii, kama vile masuala ya kimaadili na kama masuala ya kiutamaduni.
Jambo la muhimu na la kimsingi katika suala la uchumi, ni suala la uzalishaji wa bidhaa wa ndani ya nchi; ni suala la kuandaa nafasi za kazi na kuondoa ukosefu wa kazi; ni suala la kuimarisha na kustawisha uchumi na kupambana na mdororo wa uchumi; hayo ni masuala ambayo wananchi wanakabiliana; hivi ndivyo vitu ambavyo wananchi wanavihisi na wanavitaka na hata takwimu na matamshi ya viongozi wenyewe nchini yanaonesha kuwa, haya ndiyo matakwa ya wananchi na kwa hakika matakwa hayo ni sahihi na ni ya mahala pake kabisa.
Kama tunataka kutatua tatizo la kuzora uchumi na ili tuweze kutatua tatizo la uzalishaji wa bidhaa za ndani na tutatue pia suala la ukosefu wa ajira, kama tutataka kudhibiti mambo yote hayo, basi tujue kuwa utatuzi wa masuala yote hayo unapatikana katika majimui ya mapambano ya kiuchumi na katika uchumi ngangari na wa kusimama kidete. Uchumi ngangari na wa kusimama kidete unajumuisha mambo yote hayo. Inawezekana kupambana na ukosefu wa kazi kupitia uchumi ngangari; inawezekana kupambana na kuzorota kwa uchumi kwa kutumia uchumi ngangari, kama ambavyo inawezekana pia kupambana na ughali wa maisha; kukabiliana na vitisho vya maadui na kusimama kidete kupitia uchumi huo; inawezekana kuiandalia nchi fursa nyingi na kuzitumia vizuri fursa hizo kwa sharti kwamba tuufanyie kazi uchumi ngangari na wa kimapambano na tujitahidi kuufanikisha kivitendo na inavyotakiwa.
Ripoti ambazo wamenipa ndugu zetu serikalini zinaonesha kuwa, wamefanya kazi kubwa, lakini yote hayo ni utangulizi tu. Kazi za kuandaa miswada na ajenda za sekta tofauti; hizo ni kazi za utangulizi tu. Jambo la lazima hapa ni kuendelezwa kazi hizo, jambo la lazima ni kuchukuliwa hatua na kutekelezwa kivitendo mambo hayo, ili wananchi waweze kuona matunda yake; hili ndilo jukumu letu; na Inshaallah nitalitolea ufafanuzi zaidi suala hilo wakati nitakapozungumza na wananchi wetu azizi wa matabaka tofauti.
Kwa kuzingatia yote hayo nimeona nara na kaulimbiu yetu mwaka huu iwe ni "Uchumi Ngangari, Hatua na Vitendo." Hii ni njia na barabara iliyonyooka kuelekea kwenye kitu tulichokikusudia. Sitegemei kuwa hatua na vitendo hivyo vitaweza kumaliza matatizo yote katika kipindi cha mwaka mmoja; lakini nina yakini kwamba, kama hatua na vitendo vitafanyika kwa mpangililio mzuri na kwa utekelezaji sahihi, basi matunda na athari ya jambo hilo tutaziona waziwazi mwishoni mwa mwaka huu. Ninawashukuru watu wote waliofanya juhudi na wanaoendelea kufanya juhudi katika njia hii.
Kwa mara nyingine ninatuma salamu zangu na mkono wa sikukuu kwa taifa letu azizi nikimuombea rehema na amani Mtume wetu Muhammad na Aali Muhammad pamoja na Imam Mahdi (Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake, na roho zetu ziwe wahanga wake.)
Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh